Sudan yaripoti wagonjwa wa kipindupindu zaidi ya elfu 43
Sudan jana Alhamisi iliripoti watu zaidi ya 43,000 wanaugua kipindupindu huku wengine 1,800 wakiaga dunia kwa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa wagonjwa wapya wa kipindupindu 221 wamebainika katika majimbo nane ya nchi hiyo wakiwemo wagonjwa wawili waliopoteza maisha; na hivyo kuifanya idadi jumla ya wagonjwa wa kipindupindu kote nchini humo kufikia 43,490.
Taarifa ya Wizara ya Afya ya Sudan imeeleza kuwa wagonjwa wa kipindupindu wamemepatikana huko Khartoum, Al Jazira, Al Qadarif, Kassala, Katika jimbo la Mto Nile, Jimbo la Kaskazini, White Nile na Sennar.
Aidha wizara hiyo imearifu kuwa kesi mpya 15 za homa ya dengue zimeripotiwa pia na hivyo kuzidisha idadi ya maambukizi hadi 8,008 na vifo 16.
Homa ya dengue, inayoambukizwa kwa kuumwa na mbu husababisha dalili kama vile homa kali, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli na viungo, kichefuchefu na kutapika.
Sudan imekumbwa na mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa kikosi cha msaada wa haraka (RSF) tangu Aprili 2023.