Sudan yaikosoa EU kwa kuwawekea vikwazo majenerali wake 2
-
Jenerali Abdul Fattah al Burhan
Sudan imelaani uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuwawekea vikwazo majenerali wawili wa jeshi la nchi hiyo, ikieleza kuwa hatua hiyo ni potofu na yenye dosari.
Umoja wa Ulaya, Jumatatu wiki hii uliwaweka Wasudani wanne katika orodha yake ya vikwazo kwa kile ilichokitaja kuwa "kutishia amani na usalama wa nchi."
Watu hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Intelijinsia wa Jeshi la Sudan, Jenerali Mohamed Ali Ahmed Sabir, na mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Salah Abdallah. Wengine wawili ni makamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Mapigano yanaendelea kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF nchini humo tangu Aprili mwaka jana.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imelaani vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya majenerali wawili wa jeshi la nchi hiyo, ikisema uamuzi huo "hauna msingi" na unaonyesha "mtazamo mbovu na usio sahihi wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu mzozo unaoendelea Sudan.
Taarifa ya wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imezitaka nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kubadili uamuzi wao kuhusu Sudan ili kupatia ufumbuzi wa kile kinachoendelea nchini humo, na kuchukua "msimamo chanya" wa kuiunga mkono Sudan katika kukabiliana na "mashambulizi na hujuma za ugaidi."