Nchi za Magharibi zina nafasi gani katika kuongezeka ugaidi Afrika?
Kuongezeka kwa shughuli za kigaidi katika maeneo mbalimbali ya Afrika kumegeuka kuwa tatizo kubwa katika bara hilo na pia katika mataifa mengi duniani. Hivi sasa, makundi kadhaa ya kigaidi yanaendesha shughuli zao katika maeneo tofauti ya Afrika.
Vasily Nebenzya, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amesema kwamba makosa katika uga wa usalama na hatua zisizo halali za nchi za Magharibi zimechangia kwa kiasi kikubwa kusambaa kwa ugaidi barani Afrika.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu ugaidi barani Afrika, Nebenzya ameeleza kuwa mataifa ya Afrika yalishuhudia kuongezeka kwa ugaidi wa kimataifa baada ya uvamizi wa kijeshi wa madola ya Magharibi nchini Libya mwaka 2011. Hujuma hiyo dhidi ya Libya iliyoongozwa na muungano wa kijeshi wa NATO iliandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya makundi ya kigaidi kuimarika na kusambaa kote barani Afrika.
Shughuli za makundi ya kigaidi kama al-Shabaab katika eneo la Afrika Mashariki, hasa Somalia, na Boko Haram huko Afrika Magharibi, pamoja na makundi mengine kama ISIS au Daesh katika Ukanda wa Sahel, zimekuwa zikivuruga usalama wa nchi mbalimbali za Afrika kwa muda mrefu. Kulingana na makadirio, zaidi ya magaidi 10,000 kutoka makundi mawili makubwa, ISIS na al-Qaeda, wanapatikana barani Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, kuongezeka kwa makundi ya kigaidi kumetokana na changamoto za kisiasa na kiuchumi katika nchi za Afrika ambazo zimetokana na ukoloni mamboleo wa nchi za Magharibi. Mgogoro wa Libya, ambao ulitokana na sera za uingiliaji wa Magharibi, unachukuliwa kuwa sababu kubwa ya kuenea kwa ugaidi Afrika.
Nebenzya amesisitiza kwamba nchi za Magharibi ziliharibu serikali na uchumi wa Libya kwa kisingizio cha kuilinda nchi hiyo. Hujuma ya NATO dhidi ya Libya ilitoa nafasi kwa makundi ya kigaidi kuimarika na kusambaa barani humo.
Baada ya kuangushwa Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya, taifa lenye umuhimu wa kijiografia na rasilimali nyingi za mafuta na gesi, lilikumbwa na hali ya kutoaminiana kisiasa. Mgogoro wa ndani kati ya makundi ya kisiasa ya Libya unaendelea hadi leo, na nchi hiyo imegeuka kuwa kituo cha ugaidi unaoathiri mataifa mengine ya Afrika kama Tunisia, Niger na Mali.
Aidha, kuongezeka kwa hali ya ukosefu wa usalama barani Afrika kumezipa nchi za Magharibi kisingizio cha kuwepo kijeshi katika bara hilo. Katika kipindi cha karibu miaka 20 iliyopita, Ufaransa ilianzisha kambi za kijeshi katika nchi za Sahel kama Mali na Niger kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Wanajeshi kutoka nchi nyingine za Ulaya kama Ujerumani pia wamekuwa katika bara hili kwa kisingizio hicho hicho.
Ingawa nchi za Ulaya na Marekani zimekuwa barani Afrika kwa zaidi ya muongo mmoja kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, juhudi za dhati za kuondoa ugaidi hazijachukuliwa. Badala yake, wamekuwa wakitumia bara hili kama njia ya kufikia malengo yao ya kiuchumi na kimkakati.
Vita kama vya Ukraine na Russia pia vimechangia hali hii. Silaha zinazotumwa Ukraine na nchi za Magharibi zimekuwa zikipatikana mikononi mwa makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel. Isaa Konfourou, Mwakilishi wa Mali katika Umoja wa Mataifa, alionya kuwa silaha hizi zimeongeza uhalifu, ugaidi na vurugu katika eneo hilo.
Kukua kwa makundi ya kigaidi sasa ni tishio kubwa kwa mataifa yote. Kwa mujibu wa Brett Holmgren, mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani, ISIS imefanya Afrika kuwa eneo jipya la operesheni zake, na shughuli zake barani zimekuwa hatari zaidi.
Ripoti hii inasisitiza kwamba miaka mingi ya uwepo wa majeshi ya kigeni Afrika haijaleta suluhisho lolote kwa tatizo la ugaidi. Badala yake, imechangia katika kuimarika kwa makundi ya kigaidi, na hivyo kuendelea kutumika bara hili kwa maslahi binafsi . ya madola ya Magharibi