Sudan kukabiliana na watakaojaribu kuunda serikali nyingine
Mjumbe wa Baraza Kuu la Sudan amesema serikali ya nchi hiyo "itapambana na yeyote anayetaka kuanzisha serikali nyingine" katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Shirika rasmi la habari la Sudan (SUNA) limemnukuu Yasser Al-Atta, Mjumbe wa Baraza Kuu la Sudan akisema hayo alipokuwa akiwahutubia wanajeshi katika mji wa Al Dabba kaskazini mwa Sudan na kuongeza kuwa, "Kwa wale wanaosema wataunda serikali yao, tutapambana nao katika kila shibri ya ardhi ya Sudan."
Matamshi ya Al-Atta, ambaye pia anahudumu kama msaidizi wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan yamekuja saa chache baada ya kufanyika kikao cha ufunguzi wa mkutano uliopewa jina la "The Founding Alliance of Sudan" huko Nairobi, Kenya. Mkutano huo uliandaliwa na vikosi vya upinzani na makundi yenye silaha yanayopambana na jeshi la Sudan, kwa lengo la kuunda serikali yao.
Serikali ya Sudan imeshutumu vikali Kenya kwa kuruhusu Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuandaa mkutano huo katika Jumla la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, na kuitaja hatua hiyo kuwa ya uhasama.
Katika hatua nyingine, zaidi ya raia 200 wasiokuwa na ulinzi wamedaiwa kuuawa na wapiganaji wa RSF katika vijiji tofauti vya Sudan katika kipindi cha siku tatu zilizopita. Shirika la kutetea haki za binadamu katika eneo hilo la Emergency Lawyers limesema, mauaji hayo yalitokea katika vijiji vya al-Kadaris na al-Khelwat kaskazini mwa jimbo la White Nile; maeneo ambayo hayana wanajeshi wa serikali.
Mtandao huo wa kutetea haki za binadamu umesema, "Wapiganaji wa RSF wana hatia ya "kunyonga, utekaji nyara, kupotazana kwa nguvu na uporaji wa mali." Makumi ya maelfu ya raia wameuawa nchini Sudan tokea Aprili 2023, huku RSF na jeshi wakituhumiwa kufanya ukatili.