RSF yaua raia 23 katika mashambulizi kadhaa al-Jazira, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123610-rsf_yaua_raia_23_katika_mashambulizi_kadhaa_al_jazira_sudan
Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) vimeripotiwa kuwauwa makumi ya raia katika vijiji vya jimbo la al-Jazira ambalo linapakana na mji mkuu Khartoum, kaskazini mwa nchi.
(last modified 2025-03-07T07:30:48+00:00 )
Mar 07, 2025 07:30 UTC
  • RSF yaua raia 23 katika mashambulizi kadhaa al-Jazira, Sudan

Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) vimeripotiwa kuwauwa makumi ya raia katika vijiji vya jimbo la al-Jazira ambalo linapakana na mji mkuu Khartoum, kaskazini mwa nchi.

Katika taarifa tofauti, mashirika mawili ya kijamii ya Kongamano la al-Jazira na Jukwaa la Nidaa Al-Wasat, yamesema kwamba, raia 23 waliuawa Jumatano na jana Alkhamisi katika vijiji vya Al-Baqir na eneo la al-Jadeed al-Thawra kutokana na mashambulizi ya RSF.

Kwa mujibu wa Nidaa al-Wasat, RSF iliweka kijiji cha Habiba chini ya mzingiro, na kuwazuia wakazi kuondoka. “Kijiji kinaomboleza vifo vya mashahidi saba,” imesema taarifa hiyo.

Pia iliripoti majeruhi katika maeneo mengine: sita waliuawa, ikiwa ni pamoja na mwanamke na mtoto katika eneo la al-Jadeed al-Thawra, wanane waliuawa ikiwa ni pamoja na mwanamke katika kijiji cha Al-Jadeed Al-Qahwa, na wawili waliuawa huko Al-Farajin.

"Mashahidi saba kutoka kijiji cha Habiba walipigwa risasi na kuuawa na vikosi vya RSF wakati wa sala ya (Muslim) Tarawih siku ya Jumatano," Kongamano la Al-Jazira limesema.

Hivi majuzi, jeshi la Sudan lilifanikiwa kudhibiti takriban jimbo lote la al-Jazira isipokuwa vijiji vidogo vya kaskazini na kaskazini magharibi karibu na Khartoum.

Katika wiki chache zilizopita, RSF imepoteza eneo muhimu kwa jeshi la serikali katika majimbo ya Khartoum, al-Jazira, Kordofan Kaskazini, White Nile, Sennar na Blue Nile.