Zimbabwe: Tunafanya hima kujiunga na kundi la BRICS
(last modified Sat, 08 Mar 2025 07:01:11 GMT )
Mar 08, 2025 07:01 UTC
  • Zimbabwe: Tunafanya hima kujiunga na kundi la BRICS

Zimbabwe inafanya kila liwezekanalo kujiunga na kundi la BRICS, ikilenga kuimarisha uchumi wake na ushirikiano wa kimataifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, Amon Murwira baada ya ziara yake mjini Moscow ambapo ameeleza kuwa, Zimbabwe inatazamia kushirikiana na makundi kama vile BRICS kwa shabaha ya kukuza uchumi wake.

Katika mahojiano na televisheni ya ZBC, Murwira amebainisha kuwa, "Kwa mujibu wa Katiba yetu, hatuna budi si tu kuwa wanamajimui wa Afrika (Pan-African), lakini pia tujiunge na vikundi vya kimaendeleo ambavyo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, na kwa ajili ya kuendeleza amani duniani."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Zimbabwe ameeleza kuwa: Kwa kawaida amani hustawishwa kupitia maendeleo ya kiuchumi, lakini pia tunapaswa kuwa pamoja na watu wa mataifa mengine.

Amesema Zimbabwe iko tayari kujiunga na jumuiya ya kiuchumi ya BRICS, ambayo itatoa fursa nzuri kwa nchi hiyo kufanya biashara katika mazingira huru na nchi nyingine wanachama.

Huko nyuma pia, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe alitangaza azma ya nchi yake kujiunga na BRICS, katika mahojiano na shirika la TASS pambizoni mwa mkutano wa kiuchumi wa St. Petersburg International Economic Forum (SPIEF).