Watalii kadhaa wafa maji baada ya nyambizi kuzama katika Bahari Nyekundu
Raia sita wa Russia wamepoteza maisha huku watalii 39 wa kigeni wakiokolewa wakati nyambizi ya kitalii ilipozama kwenye eneo la kitalii la Hurghada kwenye maji ya Bahari Nyekundu pwani ya Misri.
Hayo yamesemwa na Ofisi ya Gavana wa eneo hilo kwenye taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na kuongeza kuwa, abiria na wafanyakazi wote waliokuwa kwenye chombo hicho wameshapatikana na kutambuliwa.
Utawala wa eneo la Bahari Nyekundu umesema nyambizi hiyo yenye jina la "Sindbad" ilikuwa na watu 50 ndani yake: Watalii 45 wa mataifa tofauti wakiwemo kutoka Russia, India, Norway, na Sweden, na wafanyakazi watano wa Misri.
"Wengi wa waliokuwa kwenye chombo hicho waliokolewa na kupelekwa kwenye hoteli na hospitali huko Hurghada," ubalozi mdogo wa Russia huko Hurghada umesema.
Habari zaidi zinasema kuwa, nyambizi hiyo yenye madirisha makubwa ya kuwawezesha abiria kuona matumbawe ya kuvutia ya Bahari Nyekundu na viumbe vya baharini, ilishuka hadi kina cha mita 25 chini ya bahari.
Bahari Nyekundu ni kitovu kikuu cha tasnia muhimu ya utalii ya Misri, na nguzo ya uchumi wa nchi hiyo, ambapo ongezeko la watalii wa Russia ni sehemu kubwa na muhimu ya sekta hiyo.
Hali kadhalika, Misri huvutia watalii na piramidi zake kubwa za Giza na safari za baharini kwenye Mto Nile huko Luxor na Aswan.