Kipindupindu chaua watu zaidi ya 170 ndani ya wiki moja Sudan
Zaidi ya watu 170 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu ndani ya wiki moja katika nchi ya Sudan iliyogubikwa na mapigano kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Wizara ya Afya ya Sudan ilisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, watu 2,700 wamekumbwa na ugonjwa huo katika kipindi cha wiki moja tu, ambapo 172 miongoni mwao wameaga dunia.
Wizara hiyo imesema asilimia 90 ya kesi za kipindupindu zimerekodiwa katika Jimbo la Khartoum, ambapo nishati na usambazaji wa maji ulitatizwa katika wiki za hivi karibuni huku kukiwa na mapigano kati ya jeshi la serikali na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde zilizotolewa na wizara hiyo, jumla ya wagonjwa wa kipindupindu nchini Sudan wamefikia 60,993, na vifo 1,632. Mnamo Agosti 2024, mamlaka ya Sudan ilitangaza kipindupindu kuwa janga la kitaifa.
Haya yanaripotiwa siku chache baada ya jeshi la Sudan kutangaza mapema mwezi huu kwamba limerejesha udhibiti wa Khartoum na kuwafurusha wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Sudan, Haitham Mohamed Ibrahim, ongezeko la hivi karibuni zaidi la ugonjwa wa kipindupindu ni kubwa mno kiasi kwamba, kwa wiki kesi 600 hadi 700 za ugonjwa huo zinaripotiwa
Tangu Aprili 2023, RSF imekuwa ikipambana na jeshi kwa ajili ya udhibiti wa Sudan, na kusababisha maelfu ya vifo mbali na watu milioni 15 kukimbia makazi yao.