Maelfu ya wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekimbilia nchini Chad
Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza kuwa maelfu ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekimbilia nchini Chad.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo zaidi ya raia elfu sita wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wapo kusini mwa Chad chini ya usimamizi wa Kamisheni Kuu ya Wakimbizi iliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UNHCR). Kadhalika OCHA imesema kuwa, wakimbizi hao walikimbi makazi yao kuanzia tarehe 12 Juni mwaka huu baada ya kushadidi mapigano kaskazini mwa nchi yao.
Zaidi ya wakimbizi elfu 91 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekuwepo katika kambi za kusini mwa Chad kwa miaka kadhaa sasa.
Itakumbukwa kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikumbwa na machafuko ya ndani mwezi Disemba mwaka 2012, ambayo yalipelekea kuoanguka serikali ya wakati huo ya rais François Bozizé. Raia wa nchi hiyo wanataraji kwamba kuchaguliwa Serikali na Bunge jipya, kutaandaa mazingira ya wao kurejea nchini kwao.