Mashambulizi ya RSF yaua raia 16 eneo la Kordofan, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134504-mashambulizi_ya_rsf_yaua_raia_16_eneo_la_kordofan_sudan
Takriban watu 16 wameuawa katika shambulio la mizinga la waasi wa RSF lililolenga mji uliozingirwa katika eneo la Kordofan nchini Sudan, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vikiingia katika awamu hasasi kwenye mwaka wake wa tatu.
(last modified 2025-12-19T23:07:13+00:00 )
Dec 19, 2025 23:07 UTC
  • Mashambulizi ya RSF yaua raia 16 eneo la Kordofan, Sudan
    Mashambulizi ya RSF yaua raia 16 eneo la Kordofan, Sudan

Takriban watu 16 wameuawa katika shambulio la mizinga la waasi wa RSF lililolenga mji uliozingirwa katika eneo la Kordofan nchini Sudan, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vikiingia katika awamu hasasi kwenye mwaka wake wa tatu.

Wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) na washirika wao wanachama wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini (SPLM-N) walishambulia maeneo ya makazi ya Dilling huko Kordofan Kusini kuanzia Alkhamisi na jana Ijumaa, kwa mujibu wa Mtandao wa Madaktari wa Sudan.

Wanawake, wazee na watoto walikuwa miongoni mwa raia waliouawa katika kile kikundi hicho cha madaktari na wahudumu wa afya wa Sudan kimeitaja kama hujuma ya makusudi dhidi ya raia.

Shambulio hilo dhidi ya mji wa Dilling ni sehemu ya kampeni inayoongezeka ya mapigano kote Kordofan ambayo imewaua zaidi ya raia 100 tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Desemba, huku mapigano katika vita vya Sudan yakihama kutoka eneo la magharibi mwa Darfur hadi eneo la kimkakati la kati.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuyashinikiza makundi yote mawili yenye silaha kusitisha mara moja mashambulizi katika maeneo ya raia na kuhakikisha ufikaji wa misaada ya kibinadamu kwa wale walionasa kwenye mapigano hayo.

Sudan ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili 2023 kutokana na uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF. Vita hivyo, ambavyo hivi sasa viko katika mwaka wake wa tatu, vimeshaua zaidi ya watu 40,000.