Somalia yazuia meli za Israel kupita Bab al-Mandab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i137902-somalia_yazuia_meli_za_israel_kupita_bab_al_mandab
Somalia imepiga marufuku meli za utawala wa Israel kupita katika mlango‑bahari wa kimkakati wa Bab al‑Mandab kama jibu kwa hatua ya utawala huo ya kulitambua rasmi eneo lililotangaza kujitenga na Somalia la “Somaliland”.
(last modified 2026-04-23T09:54:19+00:00 )
Apr 23, 2026 09:47 UTC
  • Abdullahi Warfa
    Abdullahi Warfa

Somalia imepiga marufuku meli za utawala wa Israel kupita katika mlango‑bahari wa kimkakati wa Bab al‑Mandab kama jibu kwa hatua ya utawala huo ya kulitambua rasmi eneo lililotangaza kujitenga na Somalia la “Somaliland”.

Idara ya habari za kimataifa ya shirika la habari la Fars imetangaza kuwa: “Abdullahi Warfa”, balozi wa Somalia huko Ethiopia na pia katika Umoja wa Afrika, akijibu hatua ua utawala wa kizayuni wa Israel ya kutambua rasmi kujitenga eneo la Somaliland, ameonya kwamba aina yoyote ya kuingilia mamlaka ya Mogadishu itasababisha madhara makubwa. 

Warfa ameongeza kuwa nchi yoyote itakayoingilia masuala ya ndani ya Somalia na kuathiri ukamilifu wa ardhi na mamlaka yake itakabiliana na matokeo mabaya, yakiwemo vizuizi vya kupita katika mlango‑bahari wa Bab al‑Mandab. 

Ijapokuwa wachambuzi wanahoji uwezo wa Somalia — ambayo haina jeshi la majini au la anga lenye nguvu — wa kutekeleza kijeshi marufuku hiyo, lakini wanasisitiza kwamba msimamo huu unaweza kuwa na athari hatari za kidiplomasia, na huenda ukaisukuma Mogadishu kuelekea upande wa kuanzisha uhusiano mpya na Sana’a; jambo ambalo linaweza kuhatarisha uhusiano wa Somalia na Marekani. 

Mabadiliko haya yanajiri siku chache baada ya utawala wa kizayuni wa Israel kuanza kutekeleza makubaliano ya kubadilishana mabalozi na eneo la Somaliland, na kuwa utawala wa kwanza kulitambua eneo hilo kama nchi huru tangu lilipotangaza kujitenga na Somalia mnamo mwaka 1991. 

Hatua hii ya Israel inakuja ilhali Somaliland haijatambuliwa na Umoja wa Mataifa wala nchi yoyote kama dola huru yenye mamlaka kamili.