Uganda yapitisha sheria ya kudhibiti ushawishi wa kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138450-uganda_yapitisha_sheria_ya_kudhibiti_ushawishi_wa_kigeni
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametia saini sheria mpya inayolenga kudhibiti ushawishi wa kigeni nchini humo.
(last modified 2026-05-18T12:35:02+00:00 )
May 18, 2026 12:03 UTC
  • Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
    Rais wa Uganda, Yoweri Museveni

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametia saini sheria mpya inayolenga kudhibiti ushawishi wa kigeni nchini humo.

Sheria hiyo, inayojulikana kama Sheria ya Kulinda Mamlaka ya Taifa, inaweka masharti makali kuhusu shughuli zinazohusishwa na maslahi ya kigeni. Inawataka watu binafsi na taasisi zinazofanya kazi kwa niaba ya taasisi za kigeni kujisajili kwa mamlaka husika. Aidha, sheria hiyo inaharamisha vitendo vinavyoonekana kukuza maslahi ya nje kuliko vipaumbele vya taifa.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ukiukaji unaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka kumi jela pamoja na faini kubwa za kifedha.

Mfumo huu mpya wa kisheria unalenga shughuli mbalimbali zinazohusishwa na ushawishi wa kigeni. Unazuia ushiriki katika uundaji wa sera za serikali kwa watu au makundi yenye uhusiano na taasisi zenye kulinda maslahi ya kigeni isipokuwa kwa idhini ya serikali.

Vilevile, sheria inahitaji mawakala wa kigeni kujisajili rasmi na inaweka mipaka ya kisheria kazi za zinazohusiana na mashirika ya kimataifa au wafadhili wa kigeni.

Wafuasi wa sheria hiyo wanasema inalenga kuimarisha uhuru wa taifa na kupunguza mashinikizo ya kisiasa kutoka nje.

Rais Museveni amepuuza tamko la Benki ya Dunia ambayo ilikosoa sheria hiyo kwa madai kwamba eti inaweza kuzuia shughuli za kawaida za maendeleo na za kibinadamu kutokana na upana wa tafsiri inayotumika kuelezea “ushiriki wa kigeni.”

Sheria hiyo inaakisi mwelekeo unaoonekana kuongezeka duniani, ambapo serikali za nchi mbalimbali zinajaribu kurejesha udhibiti juu ya shughuli za kisiasa na maendeleo zinazofadhiliwa na vyanzo vya nje kwa misingi ya kulinda mamlaka ya taifa na usalama wa kitaifa.