Kampeni zamalizika Uganda, uchaguzi Alkhamisi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1399-kampeni_zamalizika_uganda_uchaguzi_alkhamisi
Nchini Uganda kampeni za uchaguzi zilimalizika Jumanne huku wagombea wa viti vya urais na ubunge wakijitayarisha kwa ajili ya upigaji kura siku ya Alkhamisi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2016 03:33 UTC
  • Kampeni  zamalizika Uganda, uchaguzi Alkhamisi

Nchini Uganda kampeni za uchaguzi zilimalizika Jumanne huku wagombea wa viti vya urais na ubunge wakijitayarisha kwa ajili ya upigaji kura siku ya Alkhamisi.

Kuna wagombea wanane wanaowania kiti cha urais katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambapo rais wa sasa Yoweri Museveni ametabiriwa kushinda katika uchaguzi huo.

Akizungumza katika mkutano wa mwisho wa kampeni katika Uwanja wa Kololo mjini Kampala, Rais Museveni ameahidi kuwa uchaguzi mkuu utakuwa wa amani na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kuzusha vurugu ataadhibiwa vikali.

Rais Museveni amesisitiza haja ya kudumishwa amani na utulivu wa nchi na kusema hii itasaidia kuhimiza maendeleo na kudumisha mafanikio ambayo yamepatikana hadi leo.

Mapambano yalitokea juzi kati ya polisi wa Uganda na wafuasi wa mgombea urais wa chama cha upinzani kwenye sehemu ya katikati ya mji wa Kampala, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wengi kujeruhiwa.

Jumatatu hiyohiyo polisi ya Uganda ilimtia mbaroni na kisha kumuachilia huru Dakta Kizza Besigye mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi ujao mwanasiasa ambaye anahesabiwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni.

Mgombea huru Amama Mbabazi pia anatazamiwa kutoa ushindani mkubwa kwa Museveni na Besigye katika uchaguzi huo.