Kenya: Tumemuua kamanda wa Intelijinsia wa Al-Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1483-kenya_tumemuua_kamanda_wa_intelijinsia_wa_al_shabab
Jeshi la Kenya limetangaza kuwa limemuua kamanda mkuu wa kikosi maalumu cha kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab la Somalia ambaye anaaminika kuwa ndiye aliyepanga shambulio hatari la mwezi uliopita dhidi ya kambi ya wanajeshi wa Kenya huko kusini mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2016 11:36 UTC
  • Kenya: Tumemuua kamanda wa Intelijinsia wa Al-Shabab

Jeshi la Kenya limetangaza kuwa limemuua kamanda mkuu wa kikosi maalumu cha kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab la Somalia ambaye anaaminika kuwa ndiye aliyepanga shambulio hatari la mwezi uliopita dhidi ya kambi ya wanajeshi wa Kenya huko kusini mwa Somalia.

Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Kenya (KDF) imeeleza kuwa vikosi vya jeshi hilo vinavyohudumu katika vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) vilimuua Mohamed Karatey, Naibu Kamanda Mkuu wa Al-Shabab na mkuu wa Intelijinsia wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri katika mahafali ya kuhitimu mafunzo wanamgambo wa kundi hilo yaliyofanyika tarehe 8 ya mwezi huu wa Februari.

Taarifa ya KDF imeongeza kuwa inaaminika Karatey alikuwa na nafasi kubwa katika shambulio la karibuni huko El Adde kwa kutuma washambuliaji wake wa kujitoa mhanga. "Kuuawa kwake kunajumuisha na kuuawa kwa Abdi Dek, kamanda wa oparesheni wa Brigedi ya Abu Zubeyr iliyotekeleza shambulio la El Adde", imeongeza taarifa hiyo ya jeshi la Kenya.

Taarifa ya jeshi la Kenya haikufafanua kwa undani jinsi Karatey alivyouawa lakini imeongeza pia kwamba katika shambulio hilo la Februari 8 wanajeshi wake waliwaua pia makuruta 42 wa Al-Shabab pamoja na makamanda 10 wa ngazi ya kati.

Vikosi vya Kenya vilipata pigo kubwa wakati kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab liliposhambulia kambi ya El Adde karibu na mpaka wa Kenya tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Januari, japokuwa KDF haijatangaza hadi sasa idadi halisi ya askari waliouawa katika shambulio hilo. Kundi la Al-Shabab limedai kuwa liliua zaidi ya askari 100 wa jeshi la Kenya katika shambulio hilo.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab lenye mfungamo na mtandao wa al Qaeda linataka kuiangusha serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za Magharibi na kuvitimua katika ardhi ya nchi hiyo vikosi vya AMISOM vinavyotoa msaada wa kulinda amani na kutoa msukumo kwa jeshi la serikali ya Mogadishu katika mapambano dhidi ya kundi hilo.../