Polisi Uganda: Besigye ataachiwa huru baada ya kutangazwa matokeo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1558-polisi_uganda_besigye_ataachiwa_huru_baada_ya_kutangazwa_matokeo
Polisi nchini Uganda imesema itaendelea kumzuilia mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha FDC, Dakta Kizza Besigye na kwamba huenda akaachiwa huru hapo kesho baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais na bunge kutangazwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2016 11:35 UTC
  • Polisi Uganda: Besigye ataachiwa huru baada ya kutangazwa matokeo

Polisi nchini Uganda imesema itaendelea kumzuilia mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha FDC, Dakta Kizza Besigye na kwamba huenda akaachiwa huru hapo kesho baada ya matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais na bunge kutangazwa.

Andrew Felix Kaweesi, Kamanda Mkuu wa Polisi katika mji mkuu wa Uganda, Kampala amesema kwa mara nyingine tena wamelazimika kumkamata Besigye mapema leo ili kumzuia asizushe vurugu nchini humo, wakati huu ambapo matokeo ya uchaguzi wa rais na bunge yanaendelea kutolewa. Amesema Besige pamoja na rais wa chama cha FDC Mugisha Muntu na makada waandamizi wa chama hicho Wasswa Birigwa na Ingrid Turinawe wanazuilia katika kituo cha polisi cha Nagalama, baada ya kukamatwa katika makao makuu ya chama hicho. Polisi nchini Uganda imewaonya wafuasi wa chama hicho dhidi ya kukaribia ofisi za FDC, kutokana na kile walichokitaja kuwa 'kuzuia kubuniwa vituo bandia vya kuhesabu kura'. Kwa sasa maafisa wa usalama wameuzingira uzio wa ofisi hizo za FDC.

Hii ni katika hali ambayo, matokeo ya awali yangali yanaonesha kuwa Rais Yoweri Museveni ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miongo mitatu sasa na ambaye anawania kuhifadhi kiti hicho kupitia tiketi ya chama tawala NRM, anaongoza kwa asilimia 61.45 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa; huku mpinzani wake wa karibu Dakta Kizza Besigye akimfuata kwa asilimia 34.57.