Waasi waua wanakijiji 26 Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15595-waasi_waua_wanakijiji_26_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Msemaji wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema waasi wameua makumi ya wanakijiji katika mji mmoja ulioko katikati mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 18, 2016 11:07 UTC
  • Waasi waua wanakijiji 26 Jamhuri ya Afrika ya Kati

Msemaji wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema waasi wameua makumi ya wanakijiji katika mji mmoja ulioko katikati mwa nchi hiyo.

Mauaji hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi kufanywa katika miezi ya karibuni katika nchi hiyo inayojaribu kufungua ukurasa mpya baada ya miaka kadhaa ya machafuko yaliyochochewa na sababu za kidini na kisiasa.

Albert Mokpeme, msemaji wa Rais Faustin-Archange Touadéra amesema mauaji hayo yalitokea jana katika kijiji cha Ndomete karibu na mji wa Kaga-Bandoro ulioko katikati mwa nchi hiyo yapata kilomita 350 kutoka mji mkuu Bangui.

Mokpeme ameyahusisha mauaji hayo na kundi la waasi wa Seleka.

"Watu 26 waliuawa. Waasi walikwenda nyumba hadi nyumba.... Mkuu wa kijiji ni miongoni mwa waliouawa", amesema msemaji huyo wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Faustin-Archange Touadéra wa CAR

Imeelezwa kuwa machafuko na mapigano yanayohusisha zaidi wanamgambo wa Seleka ambao wapiganaji wake wengi ni Waislamu dhidi ya kundi la Kikristo la anti-Balaka yalianza siku ya Ijumaa huko Ndomete kabla ya kuenea hadi mjini Kaga-Bandoro.

Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA vilitumwa katika eneo la machafuko na kuyatenganisha makundi mawili hayo. Taarifa ya vikosi hivyo imeeleza kuwa MINUSCA inaimarisha doria katika maeneo yanayozunguka mji wa Kaga-Bandoro ili kuwalinda raia na kuzuia kutokea machafuko zaidi.../