Rais Touadéra: Jamhuri ya Afrika ya Kati inaelekea kwenye utulivu
Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, serikali yake imetekeleza hatua za kiusalama na kijamii.
Rais Touadéra ameyasema hayo katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kuhusiana na hali ya usalama nchini kwake baada ya miaka mitatu ya machafuko yaliyoambatana na mauaji ya umati. Amesema kuwa, serikali ya Bangui sanjari na kurejesha utawala wa kisheria, inaendelea kutekeleza hatua za kubadilisha historia nyeusi ya nchi hiyo.
Rais Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, taifa hilo limeazimia kuhitimisha kabisa machafuko na utumiaji mabavu nchini humo sambamba na kurejesha usalama, uadilifu, uhuru na ustawi. Ameahidi kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kupambana na uhalifu na ufisadi wa kifedha.
Faustin-Archange Touadéra alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Machi mwaka huu na kushika madaraka ya nchi baada ya Catherine Samba-Panza aliyekuwa rais wa mpito wa nchi hiyo kumaliza muda wake.