Mugabe: Tutawaadhibu wanaogombania kunirithi urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1618-mugabe_tutawaadhibu_wanaogombania_kunirithi_urais
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametishia kuwachukulia hatua za kinidhamu makada wa chama tawala nchini humo ZANU-PF wanaozozana kuhusu ni nani atakayerithi kiti cha urais baada yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2016 10:15 UTC
  • Mugabe: Tutawaadhibu wanaogombania kunirithi urais

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametishia kuwachukulia hatua za kinidhamu makada wa chama tawala nchini humo ZANU-PF wanaozozana kuhusu ni nani atakayerithi kiti cha urais baada yake.

Katika hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja na runinga ya taifa ya ZBC, siku mbili kabla ya kuadhimisha miaka 92 ya kuzaliwa kwake, Rais Mugabe amesema ameghadhibishwa mno na kile alichokitaja kuwa 'vita vya majibwa' na matusi miongoni mwa makada wakuu wa ZANU-PF wakivutana kuhusu nani atakayemrithi rais huyo atakapoachia uongozi. Mugabe ambaye katika hotuba yake hiyo kwa taifa alikuwa pamoja na makamu wake wawili Emmerson Mnangagwa na Phelekezela Mphoko; amesema "Hatuwezi kunyamaza kimya wakati ambapo sisi sote tunatukanwa na kuvunjiwa heshima nikiwemo mimi binafsi pamoja na mke wangu; lazima tutawachukulia hatua za kinidhamu wanachama wetu wanaohusika." Mugabe ambaye anapania kuwania urais kwa muhula wa mwisho wa tano katika uchaguzi wa mwaka 2018 ambapo atakuwa na miaka 94, amesema chama tawala ZANU-PF ndicho kitaamua mrithi wake. Hii ni katika hali ambayo, Tinomoda Chinoka, wakili wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe ametaka kuchunguzwa hali ya afya ya rais huyo ili kuwa na uhakika kuhusiana na uongozi wake.

Mahakama kuu pia imewasilisha pendekezo la Chinoka kwa spika wa bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kuchunguzwa afya na uwezo wa kimwili wa Rais Mugabe katika kuongoza nchi. Mugabe amekuwa madarakani tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza hapo mwaka 1980.