Kenya yatangaza azma ya kuangamiza kundi la kigaidi la Al Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16201-kenya_yatangaza_azma_ya_kuangamiza_kundi_la_kigaidi_la_al_shabab
Afisa wa ngazi za juu katika polisi ya Kenya amesema vikosi vyote vya usalama nchini humo vina azma imara ya kuangamiza kundi la kigaidi la Al Shabab.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 27, 2016 11:38 UTC
  • Maafisa wa kijeshi Kenya
    Maafisa wa kijeshi Kenya

Afisa wa ngazi za juu katika polisi ya Kenya amesema vikosi vyote vya usalama nchini humo vina azma imara ya kuangamiza kundi la kigaidi la Al Shabab.

Msemaji wa Polisi ya Kenya George Kinoti amenukuliwa akisema maafisa wa usalama nchini humo watafanya kila wawezalo kung'oa mizizi ya Al Shabab na kukabiliana na vitisho vyote vya usalama nchini humo.

Kinoti aidha amethibitisha habari ya kuuawa maafisa wawili wa Polisi Kenya waliotoweka wakati Al Shabab walipovamia kituo cha polisi katika kaunti ya Garissa. Amesema magaidi wa Al Shabab walichukua miili ya polisi hao na kuipeleka Somalia.

Katika hujuma hiyo ya Alkhamisi iliyopita magaidi wa Al Shabab mbali na kuua maafisa hao wa polisi pia walipora idadi kubwa ya risasi, silaha na vifaa vya mawasiliano katika kituo hicho cha polisi.

Baadhi ya duru zinasema magaidi hao walipora risasi elfu 10 na bunduki 13 za AK 47. Kundi la Al Shabab linafungamana na mtandao wa Al Qaeda na hutekeleza hujuma za mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa usalama Kenya ambapo mamia wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.