Mashirika ya misaada ya kibinadamu yasimamisha shughuli zao CAR
Mashirika kadhaa ya kutoa misaada ya kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yamesimamisha shughuli zao katika nchi hiyo kwa kile yalichokieleza kuwa, ni kushambuliwa wafanyakazi wao.
Habari kutoka Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zinasema kuwa, asasi tatu zisizo za kiserikali ambazo zimekuwa zikifanya shughuli za kutoa misaada ya kibinadamu katika mji wa Kaga-Bandoro zimeondoka katika mji huo. Inaelezwa kuwa, uamuzi huo umetokana na wafanyakazi wa taasisi hizo kushambuliwa na makundi yasiyojulikana.
Mashirika hayo yametajwa kuwa ni International Rescue Committee la Marekani, Solidarité la Ufaransa na Intersos la Italia.
Taarifa ya mashirika hayo yasiyo ya kiserikali imeeleza kuwa, hayako tayari kufanya kazi katika mazingira kama hayo ambapo wafanyazi wao wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na maisha yao kuwa hatarini.
Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulikemea hujuma na mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya misafara ya utoaji misaada katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutoa wito wa kukomeshwa vitendo hivyo.
Kusitishwa shughuli za mashirika hayo kutapelekea hali ya raia waliokuwa wakiishi kwa misaada ya asasi hizo kuwa mbaya zaidi.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko na mapigano mwaka 2013 wakati makundi ya Kikristo yanayobeba silaha yalipoanzisha mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi zaidi, ambalo mnamo mwezi Machi mwaka huo liliiondoa madarakani serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Francois Bozize.