UN: Sudan izungumzie 'kutumiwa silaha za kemikali Darfur'
Umoja wa Mataifa umeitaka Sudan ieleze msimamo wake kuhusu madai ya kutumiwa silaha za kemikali dhidi ya raia katika jimbo la Darfur.
Herve Ladsous, Mkuu wa Vikosi ya Kusimamia Amani vya Umoja wa Mataifa amesema binafsi ameshtushwa na ripoti iliyotolewa wiki jana na Amnesty International, ikidai kuwa jeshi la Sudan lilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wasiokuwa na hatia jimboni Darfur.
Wakati huo huo, Shirika la Kupambana na Matumizi ya Silaha za Kemikali (OPCW) limesema karibuni hivi litaanzisha uchunguzi kubaini iwapo madai ya Amnesty International dhidi ya serikali ya Sudan ni ya kweli au la.
Ripoti ya Amnesty International iliyotolewa Septemba 29 ilieleza kuwa, vikosi vya serikali ya Sudan vilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia baina ya mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu katika mashambulio yake dhidi ya waasi huko Darfur.
Ripoti hiyo inasema kuwa, katika mashambulio hayo kwa uchache raia 30 waliuawa huko Jabal Murrah katika jimbo la Darfur.
Kwa muda mrefu jimbo la Darfur lililoko magharibi mwa Sudan limekuwa likishuhudia machafuko na ukosefu wa usalama na kuyafanya maisha ya wakazi wa jimbo hilo kuwa hatarini.