Museveni; mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Uganda
Tume ya Uchaguzi ya Uganda juzi alasiri ilitangaza kuwa Yoweri Museveni ni Rais Mpya wa nchi hiyo baada ya kushinda zaidi ya asilimia 60 ya kura na hivyo kumshinda mpinzani wake mkuu Dakta Kiiza Besigye.
Hata hivyo Kiiza Besigye amepinga matokeo ya uchaguzi huo ambayo yamempa Museveni ushindi wa mara nyingine tena, kwa hoja kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa kimaonyesho tu.
Besigye ambaye alikuwa daktari wa Museveni wakati wa vita vya nchi hiyo, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wakati wa duru ya kwanza ya urais wa Museveni, hata hivyo mwaka 1999 alijitenga na Museveni baada ya kumtuhumu Rais huyo kuwa anakiuka demokrasia. Daktari Kiiza Besigye anatambuliwa kama mpinzani wa siku nyingi wa Yoweri Museveni na kiongozi wa wapinzani wa serikali. Besigye alikuwa mpinzani mkuu wa Rais Museveni katika uchaguzi wa Rais wa Alhamisi iliyopita.
Wakati huo huo wawakilishi wa Umoja wa Ulaya pia ambao walikuwepo nchini Uganda kusimamia uchaguzi wamesema kuwa hakukuwepo na uwazi katika utendaji wa tume ya uchaguzii ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa kundi hilo, kucheleweshwa ufikishaji wa makaratasi ya kupigia kura katika vituo vya uchaguzi khususan huko Kampala mji mkuu wa Uganda na vitongoji vyake na pia kuwepo dosari nyingine katika mchakato huo, kulisababisha uchaguzi huo kwa kiwango kikubwa kutokuwa huru wala wa kiadilifu. Wawakilishi hao vile vile wamesema kuwa polisi ya Uganda ilitumia nguvu kupita kiasi katika kumtia mbaroni kiongozi wa upinzani Kiiza Besigye.
Vikosi vya usalama vya Uganda juzi vilimuweka Besigye chini ya kifungo cha nyumbani kwa kisingizio eti cha kuzuia kuibuka ghasia zinazoweza kusababishwa na uchochezi wa Besigye kwa wafuasi wake. Masaa machache baada ya kutangazwa matokeo ya awali, raia waliopinga matokeo hayo walimiminika mitaani, hata hivyo walikabiliwa na vikosi vya jeshi.
Kwa miezi kadhaa sasa mivutano ya uchaguzi imepamba moto huko Uganda. Hatua ya kutangazwa Yoweri Museveni kuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu na kisha kuthibitishwa na Tume Kuu ya Uchaguzi ya Uganda kupeperusha bendera ya chama tawala cha NRM, kumeibua hasira za wapinzani kwa miezi kadhaa nchini humo. Wapinzani wa Uganda walimtaja Museveni kuwa dikteta mara baada ya kutangazwa kuwa mgombea wa kiti cha urais. Wapinzani hao walikituhumu chama tawala NRM kuwa kilikuwa kimeandaa mipango ya kuiba kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Malalamiko hayo ya wapinzani yameifanya Uganda katika miezi kadhaa iliyopita ikumbwe na ghasia na machafuko ya uchaguzi.
Hivi sasa pia wapinzani na khususan mgombea mkuu wa mrengo wa upinzani wamepinga matokeo ya uchaguzi huo wa Alhamisi iliyopita na kuyataja kuwa yalikusudiwa kumpatia ushindi wa mara nyingine Yoweri Museveni. Kuandaliwa mazingira ya kuwatia hofu na kuwatisha wapiga kura na wagombea wa uchaguzi, kutoandaliwa mazingira kwa ajili ya kupiga kura na kutofikishwa vifaa vya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura ni miongoni mwa ukosoaji uliotajwa na weledi wa mambo dhidi ya serikali ya Kampala. Museveni ambaye tangu miaka 30 iliyopita hadi sasa anatawala Uganda, ni kati ya Marais wa Afrika ambao mwaka 2005 walizifanyia marekebisho katiba za nchi zao kwa kufuta kipengee kinachohusiana na ukomo wa mihula miwili ya kuwepo madarakani rais wa nchi; na hivyo kujiandalia njia ya kusalia madarakani. Wapinzani wanamtuhumu Museveni kuwa anataka kuwa rais wa maisha wa Uganda.