Ufaransa yafufua uchunguzi wa mauaji ya rais wa zamani wa Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16996-ufaransa_yafufua_uchunguzi_wa_mauaji_ya_rais_wa_zamani_wa_rwanda
Ufaransa imeanzisha tena uchunguzi wa mauaji ya rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, yaliyopelekea kuanza kwa mauji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 08, 2016 10:26 UTC
  • Ufaransa yafufua uchunguzi wa mauaji ya rais wa zamani wa Rwanda

Ufaransa imeanzisha tena uchunguzi wa mauaji ya rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, yaliyopelekea kuanza kwa mauji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, jopo la uchunguzi la Ufaransa limesema kuwa linataka kumhoji Faustin Kayumba Nyamwasa, aliyekuwa mkuu wa jeshi la Rwanda kati ya mwaka 1994-2002, ili kujua iwapo alihusika katika mauaji hayo, sambamba na kumsaili juu ya maisha yake akiwa uhamishoni nchini Afrika Kusini na namna alivyoepuka majaribio mawili ya mauaji dhidi yake.

Kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Rwanda 1994

Serikali ya Rwanda imekuwa ikishikilia kwamba, Ufaransa ilihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo ya kimbari ambapo watu zaidi ya laki 8 waliuawa.

Rwanda iliwahi kuunda tume huru ya kuchunguza mauaji ya kimbari ambapo mbali na kukusanywa ushahidi wa nyaraka, lakini pia baadhi ya mashuhuda walihojiwa moja kwa moja. Matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo yalifichua kwamba, Paris kwa kutumia ushawishi wake wa kisiasa, kidiplomasia, kijeshi na kifedha ilihusika kwa kiwango kikubwa katika kuratibu na kutekelezwa mauaji hayo ya kimbari.

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Tume hiyo pia ilibaini kwamba, Ufaransa iliwapa silaha, mafunzo ya kijeshi pamoja na taarifa za kiintelijensia wapiganaji wa Kihutu kabla na wakati wa mauaji hayo.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, mauaji ya kimbari ya Rwanda yalianza Aprili 6 mwaka 1994 baada ya kuuawa rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Juvenile Habyarimana, kufuatia kutunguliwa ndege iliyokuwa imembeba karibu na uwanja wa ndege wa Kigali.