Al-Shabaab yafanya tena ukatili Kenya, yaua 12 Mandera
Watu 12 wameuawa na wengine wengi kuachwa na majeraha ya risasi baada ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kushambulia hoteli moja mjini Mandera, kaskazini mashariki mwa nchi, usiku wa jana.
Mkuu wa Polisi ya eneo la Mandera Mashariki, Ezekiel Singoe amethibitisha kutokea hujuma hiyo ya kigaidi na kusema kuwa, wanamgambo hao wa al-Shabaab walivamia Hoteli ya Bishaaro mjini Mandera na kuwaua kwa kuwafyatulia risasi watu 12 wakiwemo 10 ambao sio wakazi wa eneo hilo. Habari zinasema kuwa, magaidi hao walitumia mada za miripuko kuvunja lango kuu la hoteli hiyo na kisha kuwamiminia risasi watu walilokuwemo ndani.
Job Boronjo, Mkuu wa Polisi kaunti ya Mandera amesema vyombo vya usalama vinaendelea kutathmini shambulio hilo na kwamba watatoa takwimu rasmi za waliouwa na majeruhi baadaye leo. Imearifiwa kuwa, 10 miongoni mwa waliouawa ni wasanii ambao waliwasili Mandera jana Jumatatu, kwa ajili ya kuwatumbuiza wanafunzi wanaojiandaa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili KCSE, kupitia michezo ya tamthilia.
Haya yanajiri wiki tatu baada ya kundi hilo la kigaidi na kitakfiri kuua watu sita katika shambulio jingine la kinyama, katika eneo la Bulla Public Works, kaunti ya Mandera.
Mashambulizi ya mara kwa mara ya wanamgambo wa al-Shabaab huko Kenya na hususan maeneo ya Kaskazini Mashariki na Pwani, yamesababisha vifo vya mamia ya watu katika miaka mitatu iliyopita na pia kuathiri sekta muhimu ya utalii ya nchi hiyo.