Askari 14 wa Nigeria wauawa na Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18904-askari_14_wa_nigeria_wauawa_na_boko_haram
Kwa akali askari 14 wa jeshi la Nigeria wameuawa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika jimbo la Borno.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 06, 2016 07:42 UTC
  • Askari 14 wa Nigeria wauawa na Boko Haram

Kwa akali askari 14 wa jeshi la Nigeria wameuawa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika jimbo la Borno.

Habari zinasema kuwa, magaidi hao walivamia Kikosi cha 119 cha jeshi la Nigeria, katika kituo cha Mallam, kaskazini mwa jimbo la Borno na kuua wanajeshi hao akiwemo Luteni Kanali Muhammad Abu Ali, kamanda mkuu wa Kikosi cha 272 cha vifaru na mizinga. Aidha imearifiwa kuwa, wanajeshi la Nigeria walijibu mapigo na kuwaangamiza magaidi 19 miongoni mwao katika makabiliano makali mwishoni mwa wiki.

Wanajeshi wa Nigeria

Hujuma hiyo ya Boko Haram inaaminika kuwa ya ulipizaji kisasi, siku chache baada ya jeshi la Nigeria kutangaza kuwa limewaua wanachama wanane wa kundi hilo la kitakfiri kaskazini mashariki mwa nchi.

Novemba 2, Sani Othman Msemaji wa jeshi la Nigeria alieleza kuwa jeshi hilo limewaua wanachama wanane wa Boko Haram katika mji wa Gubio katika jimbo la Borno kufuatia operesheni mpya iliyofanywa na jeshi kaskazini mashariki mwa nchi.

Maelfu ya watu wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wameuawa katika kipindi cha miaka sita cha kujiri hujuma na mashambulizi ya Boko Haram nchini humo.

Mmoja wa mabinti wa Chibok aliyepatina akiwa na mtoto

Huku hayo yakiarifiwa, binti mmoja miongoni mwa mamia ya wasichana waliotekwa nyara na kundi hilo katika mji wa Chibok mwaka 2014, ameokolewa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Pulka, eneo la Gwoza. Habari zinasema kuwa, Maryam Ali Maiyanga hata hivyo amepatikana akiwa na mtoto wa miezi 10.