Nov 08, 2016 07:22 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano mjini Galkayo, Somalia

Watu karibu 30 wameuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa katika mapigano mapya yaliyozuka kati ya vikosi vya majimbo mawili hasimu yenye mamlaka ya ndani nchini Somalia.

Hii ni licha ya makubaliano ya usitishaji mapigano kufikiwa siku chache zilizopita baina ya majimbo ya Puntland na GalMudug juu ya eneo linalozozaniwa na majimbo hayo mawili, la Galkayo.

Kanali Mohamed Aden, kamanda wa Puntland amesema askari 16 wa jimbo hilo wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa katika makabiliano hayo mapya yaliyoanza Jumapili.

Mji wa Galkayo unaozozaniwa na Puntland na Galkayo, Somalia

Naye Hirsi Yusuf Barre, Meya wa kusini mwa Galkayo amesema askari 13 wa jimbo la Galmudug wameuawa na wengine zaidi ya  20 kujeruhiwa katika makabiliano hayo.

Novemba 4, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia na mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo Michael Keating, walitoa taarifa mjini Mogadishu ya kupongeza makubaliano yaliyosainiwa baina ya Rais wa Jimbo la Puntland Abdiweli Mohamed Ali Gaas na mwenzake wa Galmudug Abdikarim Hussein Guled ya kumaliza mgogoro na machafuko katika eneo la Galkayo.

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia

Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, watu zaidi ya 20 wakiwemo raia waliuawa na wengine zaidi ya 80 elfu kulazimika kuhama makazi yao kufuatia mapigano baina ya vikosi vya majimbo mawili ya Puntland na GalMudug..

Tags