UNICEF yaonya kuhusu idadi ya watoto wakimbizi CAR
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, kati ya kila watoto watano wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, mmoja kati yao ni mkimbizi.
UNICEF imeongeza kuwa, zaidi ya wananchi laki nane na 50 elfu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ni wakimbizi. Wakimbizi hao ambao nusu yao ni wanawake na watoto wadogo, hadi hivi sasa wameshindwa kurejea katika maeneo yao na wanaishi katika mazingira magumu ndani na nje ya nchi hiyo.
Ukosefu wa usalama uliotokana na machafuko yaliyoikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati ulipelekea watu laki tisa na 20 kuwa wakimbizi mwaka 2014 na wengi wao wameshindwa kurejea makwao hadi hivi sasa.
Hivi sasa kuna wakimbizi laki tatu na 83 elfu ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati huku raia laki nne na 86 elfu wa nchi hiyo wakiendelea kuwa wakimbizi katika nchi za Cameroon, Chad, Congo Brazzaville na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Sehemu kubwa ya wakimbizi hao wako nchini Chad.
UNICEF imeongeza kuwa, watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitajia mno mashule na vituo vya afya baada ya kudhaminiwa usalama wao.
Mapigano makali yaliyoikumba Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia tarehe 5 Disemba 2013 yameisababishia nchi hiyo matatizo mengi wakiwemo mamia ya wakimbizi.