Gambia yaizuia timu ya waangalizi wa uchaguzi wa EU nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19762-gambia_yaizuia_timu_ya_waangalizi_wa_uchaguzi_wa_eu_nchini_humo
Serikali ya Gambia imekataa kuruhusu timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya EU kuingia nchini humo kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mapema mwezi ujao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2016 04:21 UTC
  • Gambia yaizuia timu ya waangalizi wa uchaguzi wa EU nchini humo

Serikali ya Gambia imekataa kuruhusu timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya EU kuingia nchini humo kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mapema mwezi ujao.

Msemaji wa EU ameeleza wasiwasi wa umoja huo baada ya waangalizi wake kutoruhusiwa nchini Gambia pasina serikali kutoa sababu zozote. Amesema Umoja wa Ulaya umepokea taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Gambia ikisema kuwa ombi la timu hiyo waangalizi wa uchaguzi  ya EU limekataliwa.

Bendera ya EU

Msemaji wa serikali ya Gambia amekataa kutoa radiamali yoyote kuhusu madai hayo ya EU, lakini ofisa katika Tume ya Uchaguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, timu ya waangalizi wa Umoja wa Afrika AU imeruhusiwa kwenda nchini humo kufuatilia uchaguzi huo wa Disemba Mosi.

Ikumbukwe kuwa, katika uchaguzi uliopita wa rais mwaka 2011, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS ilikataa kutuma timu ya waangalizi wa uchaguzi nchini Gambia, ikilalamikia ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wa serikali kabla ya kufanyika uchaguzi wenyewe.

Uchaguzi wa rais nchini Gambia, 2011

Mapema mwezi huu, ripoti ya kurasa 43 ya Human Rights Watch ilisema Rais wa Gambia Yahya Jammeh  ameviwekea mbinyo vyama vya upinzani sambamba na kuvinyima nafasi ya kufanya kampeni zao wakati huu ambapo uchaguzi wa rais unakaribia.

Rais Jammeh anaongoza Gambia kwa mkono wa chuma tangu mwaka 1994. Mwezi Aprili mwaka huu, maelfu ya wananchi wa Gambia walifanya maandamano wakimpinga rais huyo, ambapo makumi kati yao walikamatwa.