MSF: Hali ya kibinadamu Jamhuri ya Afrika ya Kati inatia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19822-msf_hali_ya_kibinadamu_jamhuri_ya_afrika_ya_kati_inatia_wasiwasi
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limeeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2016 04:38 UTC
  • MSF: Hali ya kibinadamu Jamhuri ya Afrika ya Kati inatia wasiwasi

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limeeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Augustin Majiku, afisa wa shirika hilo huko Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema hali ya kibinadamu katika nchi hiyo ndogo ya Kiafrika ni ya kutisha na inazidi kuwa mbaya kila uchao.

Amesema hafahamu serikali inamaanisha nini inaposema kuwa hali ya kimaisha inazidi kuboreka huku akisisitiza kuwa, nchi hiyo iko katika hali mbaya na inahitaji msaada wa dharura wa jamii ya kimataifa.

Faustin Archange Touadera, Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Siku chache zilizopita, Umoja wa Mataifa ulisema dola takribani bilioni tatu za Marekani zinahitajika ili kuisaidia Jamhuri ya Afrika ya Kati kujikwamua baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopeleka maelfu ya watu kuwa wakimbizi na kuliacha taifa hilo njia panda kiuchumi, kiusalama na kimaendeleo.

Hata hivyo mkutano maalumu wa kuchangisha fedha kwa ajili ya nchi hiyo mjini Brussel nchini Ubelgiji Alkhamisi iliyopita, ulifanikiwa kupata ahadi ya misaada ya dola billioni mbili kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani ambapo jamii yake ya watu wapatao milioni tano wamegawanyika katika makundi mawili hasimu kutokana na hitilafu za kidini na kikabila.