Nov 28, 2016 04:25 UTC
  • Watu 55 wauawa katika mapigano magharibi mwa Uganda

Idadi ya watu waliouawa katika mapigano yaliyozuka katika eneo moja magharibi mwa Uganda kati ya vikosi vya usalama na kundi moja lenye silaha inaripotiwa kufikia 55.

Andrew Felix Kaweesi, msemaji wa polisi ya Uganda ametangaza kuwa, wapiganaji 41 na polisi 14 wameuawa katika mapigano baina ya polisi na watu wenye silaha ambao ni wafuasi wa mfumo wa ufalme. 

Mapigano hayo yameripotiwa kutokea katika mji wa Kasese ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ripoti za kiusalama zinasema kuwa, kundi hilo lenye silaha linaendesha mapigano yenye lengo la kujitenga eneo la Rwenzururu na kuwa na mamlaka yake.

Andrew Felix Kaweesi, msemaji wa polisi ya Uganda

Vyombo vya usalama vya Uganda vimemtia mbaroni Charles Wesley Mumbere, mfalme wa Rwenzururu, ambaye vinamtuhumu kwamba, amekuwa akichochea machafuko hayo.

Hata hivyo mfalme huyo amekanusha tuhuma hizo. Aidha vyombo vya usalama vya Uganda vimetangaza kuwa, vimewatia mbaroni watu kadhaa baada ya kuvamia kasri la mfalme huyo mjini Kasese, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Vikosi zaidi vya usalama vimepelekwa Rwenzururu, eneo lililoko katika maeneo ya milima Rwenzori na kuimarisha usalama katika maeneo yote ya mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na shambulio lolote tarajiwa kutoka kwa wafuasi wa kundi hilo.

Tags