Dec 06, 2016 15:42 UTC
  • Watu 31 wauawa katika mapigano mapya Kongo DR

Makumi ya watu wameuawa katika mapigano kati ya kundi la waasi na maafisa usalama kati kati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hubert Mbingho N'Vula, Naibu Gavana wa mkoa wa Kasaï amethibitisha kutokea mapigano makali mwishoni mwa wiki katika eneo la Tshikapa mkoani hapo, kati ya kundi moja la waasi na maafisa usalama ambapo watu 31 wamepoteza maisha.

Amesema maafisa usalama 13 na waasi 18 wameuawa katika mapigano hayo, yaliyoanza baada ya kujiri mgogoro wa kung'ang'ania madaraka miongoni mwa waasi hao, ambapo maafisa usalama walilazimika kuingilia kati kudhibiti hali.

Makundi ya waasi yanayoendeleza harakati zao wakiwa misituni

Imearifiwa kuwa, mjomba na mpwa wake walianzisha mzozo huo baada ya kuzozania uongozi wa eneo hilo, na ndipo mapigano yakaripuka na vyombo vya usalama vikalazimika kuingilia kati.

Kutokuwa na uwezo jeshi la nchi hiyo na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO wa kuyasambaratisha makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kumesababisha usalama na amani uzidi kukosekana katika maeneo mengi ya Kongo DR.

Maafisa wa kofia buluu wa UN nchini DRC

Makundi kadhaa ya waasi kutoka Rwanda na Uganda pia yamekuwa yakiendesha shughuli zao katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tags