Jan 08, 2017 07:50 UTC
  • Makumi wauawa Kongo DR katika mapigano ya kikabila na jeshi

Ofisi inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imetangaza habari ya kuuawa makumi ya watu katika mapigano makali yaliyojiri katikati mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo imesema kuwa kwa akali raia 140 wameuawa tangu mwezi Agosti mwaka jana katika maeneo ya Kasaï Kaskazini na Kasaï Mashariki, katikati mwa nchi hiyo kufuatia mapigano baina ya askari wa serikali na wafuasi wa kiongozi mmoja wa kikabila.

Kamwina Nsapu, kiongozi wa kikabila, enzi za uhai wake

Kadhalika ofisi hiyo inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa imewataka viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutatua migogoro ya nchi hiyo. Kamwina Nsapu, kiongozi wa kikabila katika maeneo yaliyotajwa ya Kasaï, aliuawa tarehe 12 Agosti katika operesheni zilizofanywa na askari usalama wa serikali. 

Kamwina Nsapu, baada ya kuuawa na jeshi la serikali

Kamwina Nsapu aliyekuwa akiishi ughaibuni nchini Afrika Kusini, alirejea nchini Kongo DR mwezi Aprili mwaka jana, ambapo mfupi baadaye alisambaza mkanda wa sauti katika mitandao ya kijamii akiitisha uasi na uhuru ndani ya nchi hiyo. Siku ya Jumatano wafuasi wa kiongozi huyo wa kikabila waliuzingira mji wa Tshimbulu wenye zaidi ya wakazi laki moja na nusu. Hata hivyo saa chache baadaye askari wa serikali walifika eneo hilo na kufanikiwa kuwafurusha wanamgambo hao.

Tags