Rais wa zamani wa Burkina Faso kupandishwa kizimbani mwezi ujao
Rais wa zamani wa Burkina Faso anatazamiwa kupandishwa kizimbani mwezi ujao wa Machi, kwa kosa la kutumia mkono wa chuma kuzima maandamano dhidi ya serikali yake mwaka 2014.
Armand Ouedraogo, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Juu ya Burkina Faso ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mbali na rais wa zamani wa nchi hiyo, Blaise Compaore, maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali yake akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Luc Adolphe Tiao, watapandishwa kizimbani.
Kati ya maafisa 34 wa serikali ya Compaore, saba watahukumiwa bila ya wao kuwepo mahakamani mwezi ujao wa Machi.
Watu 33 waliuawa katika machafuko ya kumpindua Compaore mwaka Oktoba 2014, mbali na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa. Baada ya kuondolewa madarakani, Blaise Compaore alikimbilia Ivory Coast ambako alipewa uraia wa nchi hiyo.
Mwezi Disemba mwaka 2015, Burkina Faso ilitoa waranti wa kutiwa mbaroni Compaore kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya rais wa zamani wa Burkina Faso, Thomas Sankara katika mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1987.