11 wauawa katika makabiliano baina ya jeshi la Nigeria na Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25266-11_wauawa_katika_makabiliano_baina_ya_jeshi_la_nigeria_na_boko_haram
Kwa akali watu 11 wameuawa katika makabiliano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram mapema leo katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 17, 2017 14:27 UTC
  • 11 wauawa katika makabiliano baina ya jeshi la Nigeria na Boko Haram

Kwa akali watu 11 wameuawa katika makabiliano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram mapema leo katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi mwa Nigeria.

Duru za polisi nchini humo zinasema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika wamekabiliana na wanachama wa Boko Haram ambao walikuwa wanataka kutekeleza shambulizi la bomu la kujitolea muhanga kwa kujiripua karibu na kambi moja ya wakimbizi katika mji huo. 

Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi tisa wa Boko Haram wakiwemo wanawake watatu wameuawa na jeshi la Nigeria katika mapigano hayo, huku raia wawili wakipoteza maisha pia.

Ramani ya Nigeria inayoonyesha mji ulioshambuliwa wa Maiduguri

Hata hivyo baadhi ya duru za habari zinaarifu kuwa, magaidi saba miongoni mwa tisa waliofariki dunia katika makabiliano hayo, walijiua kwa kujiripia na mabomu waliyokuwa wamejifunga.

Haya yanajiri chini ya wiki tatu baada ya jeshi la Nigeria kutangaza kuwa limeendelea kusonga mbele na kupata mafanikio makubwa katika operesheni zake dhidi ya kundi la kigaidi la wanamgambo wa Boko Haram.

Kundi la Boko Haram lilianzisha harakati zake za uasi mwaka 2009 nchini Nigeria na kupanua wigo wa hujuma zake mwaka 2015 katika nchi jirani na Nigeria za Niger, Chad na Cameroon. Zaidi ya watu 20,000 wameuawa kutokana na hujuma na mashambulio ya kundi hilo huku wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita wakibaki bila ya makazi.

Magaidi wa Boko Haram