Watu 1,200 waambukizwa kipindupindu nchini Msumbiji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26394-watu_1_200_waambukizwa_kipindupindu_nchini_msumbiji
Wizara ya Afya ya Msumbiji imetangaza kwamba mamia ya watu wameathiriwa na ugonjwa wa kipindupindu katika nchi hiyo ya Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 14, 2017 22:59 UTC
  • Watu 1,200 waambukizwa kipindupindu nchini Msumbiji

Wizara ya Afya ya Msumbiji imetangaza kwamba mamia ya watu wameathiriwa na ugonjwa wa kipindupindu katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Benigna Matsinhe, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Afya ya Umma nchini humo amewaambia waandishi wa habari mjini Maputo kuwa, watu wawili wameafriki kutokana na mripuko wa ugonjwa huo, huku wengine 1,222 wakiambukizwa.

Amesema mikoa minne kati ya 13 ya nchi hiyo imeathiriwa zaidi na maradhi hayo, ambayo yalianza kusambaa kutoka mji mkuu Maputo Januari 5 mwaka huu, hususan  mkoa wa Tete, ulioko magharibi mwa mpaka wa nchi hiyo na Zimbabwe na Malawi. Ameongeza kuwa, maradhi hayo ambayo yaliua watu zaidi ya 40 mwaka 2015, yamewaathiri watu karibu 400 katika mkoa huo.

Baadhi ya wathiriwa wa ugonjwa wa kipindupindu

Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Msumbiji ametahadharisha kuwa, serikali imeshindwa kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa huo katika mikoa iliyoathirika. Msumbiji imekuwa ikishuhudia mvua kubwa tangu Oktoba mwaka jana, baada ya nchi hiyo kukumbwa na kiangazi kwa muda wa miaka miwili mfululizo.

Mapema mwezi huu, Hassan Ali Khayre, Waziri Mkuu wa Somalia alitangaza kuwa, ugonjwa wa kipindupindu uliolikumba eneo la Bay, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika umesababisha kwa akali vifo vya watu 110. 

Kadhalika mwishoni mwa mwaka uliopita 2016, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, watu 500 wamepoteza maisha yao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kutokana na ugonjwa huo.