Hali ya kibinadamu yazidi kuzorota katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa hali ya kibinadamu imeendelea kuwa mbaya katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric ameyasema hayo mjini New York, Marekani na kuongeza kuwa, zaidi ya nusu ya jamii yote ya watu wa nchi hiyo wanahitaji misaada ya kibinadamu. Amesema kuwa, machafuko yaliyoshika kasi sambamba na ongezeko la vita katika maeneo tofauti ya nchi hiyo vimewalazimisha zaidi ya watu laki moja kuyakimbia makazi yao katika kipindi cha miezi kadhaa ya hivi karibuni.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa, licha ya kuongezeka idadi ya wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini kiwango cha misaada ya kibinadamu ambayo imekuwa kitolewa nchini humo kimeendelea kupungua tangu mwaka 2014. Machafuko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliongezeka zaidi baada ya wanachama wa kundi la Seleka kumuondoa madarakani François Bozizé, rais wa zamani wa nchi hiyo hapo mwaka 2013.
Serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Faustin-Archange Touadéra imeshindwa kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo ya katikati mwa Afrika kutoka mikononi mwa wanamgambo wanaobeba silaha.