Afrika Kusini yapania kuiuzia Iran mfumo wa makombora
Mtandao wa habari wa mybroadband umeripoti kuwa Afrika Kusini inataka kuiuzia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mfumo wa makombora ya ardhini hadi angani.
Ripoti hiyo iliyonukuliwa na shirika la habari la Tasnim inasema kuwa, Afrika Kusini imelitaarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wake huo wa kuiuzia Iran mfumo wa makombora wa Umkhonto kwa gharama ya dola milioni 118 za Marekani.
Mfumo wa makombora ya ardhini hadi angani ya Umkhonto umekuwa ukitumiwa na Kikosi cha Majini cha Meko A200 class cha Afrika Kusini tangu mwaka 2001 na unahesabiwa kuwa moja ya mifumo ya makombora yenye usahihi mkubwa katika ulengaji shabaha.
Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, Disemba 13 mwaka jana, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zilitia saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi.
Hati hiyo ya maelewano ilisisitizia udharura wa kuzidishwa ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi kati ya nchi hizo mbili, kufanya jitihada za kuimarisha amani na usalama wa kikanda na kimataifa na kudumisha mapambano ya pande zote dhidi ya ugaidi.
Kadhalika ilitilia mkazo suala la ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za usalama wa baharini, masuala ya mafunzo na kubadilishana uzoefu katika medani ya kupambana na uhalifu wa kupangwa.