Ufaransa katika jitihada za kupanua mahusiano yake na Tunisia
Katika safari yake katika nchi za kaskazini mwa Afrika, Waziri Mkuu wa Ufaransa amejadili njia za kuanzisha na kuongeza ushirikiano katika uga wa kiuchumi na kuchunguza masuala mbalimbali ikiwemo migogoro ya kieneo.
Katika hatua ya pili ya safari yake kaskazini mwa Afrika Bernard Cazeneuve aliingia Tunisia jana akitokea nchini Algeria. Mazungumzo ya kupanuliwa ushirikiano wa nchi mbili hususan katika uga wa kupambana na ugaidi na masuala ya kiuchumi ni miongoni mwa malengo ya safari hiyo. Akiwa nchini Tunisia Waziri Mkuu wa Ufaransa amefanya mazungumzo na Youssef Chahed, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, ambapo amesisitizia uungaji mkono wa nchi yake kwa serikali ya Tunis katika sekta za uchumi na fedha. Bernard Cazeneuve amesema kuwa, Ufaransa itayageuza madeni ya Tunisia kuwa fursa ya uwekezaji katika sekta za miundomsingi na mipango mbalimbali ya maendeleo. Katika kikao hicho, kumetiwa saini pia makubaliano ya kibiashara yenye thamani ya Euro milioni 165.
Kadhalika mawaziri wakuu wa nchi mbili hizo wamejadili mgogoro wa Syria na kadhalika mgogoro wa kisiasa na kiusalama wa Libya. Viongozi hao wa ngazi za juu wa Ufaransa na Tunisia wamesisitizia juu ya umuhimu wa kutatuliwa mgogoro wa kisiasa nchini Libya kwa mujibu wa ubunifu wa Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia. Mpango wa Beji Caid Essebsi kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa Libya unazingatia maridhiano ya kitaifa yanayozijumuisha pande zote. Mazungumzo ya viongozi wa Tunisia na Ufaransa yamefanyika katika hali ambayo nchi hizo zinakabiliwa na matatizo mengi.
Tunisia ambayo ni moja ya nchi muhimu katika eneo la kaskazini mwa Afrika na mbeba bendera ya mwamko wa wananchi dhidi ya madikteta wa ulimwengu wa Kiarabu, kama zilivyo nchi nyingi za Kiarabu katika eneo, inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, tofauti za kisiasa na hatari ya ugaidi. Mashambulizi ya kigaidi ya miaka kadhaa iliyopita nchini Tunisia, yameathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii ambayo ni muhimili wa vyanzo vya fedha za kigeni kwa nchi hiyo. Umasikini na ukosefu wa ajira na kadhalika matatizo ya kiuchumi, ni miongoni mwa sababu zilizopelekea kuibuka harakati ya mwamko wa wananchi dhidi ya dikteta Zine El Abidine Ben Ali, rais wa zamani wa nchi hiyo.
Hata hivyo matatizo hayo bado yameendelea kuwakabili wananchi hadi sasa, kiasi cha kuwafanya viongozi kutoa ahadi za kila mara za kutatua matatizo ya kiuchumi katika fremu ya kuboresha mazingira na kuongeza uungaji mkono wa wananchi kwa serikali. Katika uwanja huo, ongezeko la mabadilishano ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa kigeni ni mambo yanayopewa kipaumbele na viongozi wa Tunisia. Kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi ni tatizo jingine katika eneo la kaskazini mwa Afrika hususan Tunisia. Kupakana na Libya na kadhalika migogoro ya kisiasa inayoshuhudiwa katika nchi nyingi za eneo hilo katika miaka michache iliyopita, ni tatizo jingine ambalo linatishia usalama wa mataifa hayo.
Kwa upande mwingine, Ufaransa pia imekuwa ikilikodolea macho ya tamaa eneo la kaskazini mwa Afrika ambapo mwamko wa wananchi dhidi ya taifa hilo la Ulaya ulihesabiwa kuwa harakati ya kuyakomboa mataifa ya eneo hilo yaliyokuwa makoloni ya zamani ya Paris. Hata hivyo Ufaransa bado inaendeleza harakati za kupenyeza zaidi katika eneo hilo kupitia ukoloni mamboleo. Katika uwanja huo, kutoa misaada ya kifedha, mafunzo ya kijeshi, kutuma askari wake kwa ajili ya eti kulinda amani na uthabiti ni kati ya njama zinazotekelezwa na viongozi wa serikali ya Paris dhidi ya nchi za Kiafrika. Hususan katika kipindi cha sasa ambapo kumeongezeka matatizo ya kiuchumi nchini Ufaransa na katika nchi za Umoja wa Ulaya na kadhalika ongezeko la vitisho vya kigaidi nchini humo, hivyo uepo wa Paris katika eneo la kaskazini mwa Afrika, ni wa kuzingatiwa na madola hayo. Hivi sasa Ufaransa imekusudia kuongeza mahusiano yake ya kiuchumi na kisiasa na nchi za eneo hususan Tunisia. Hata hivyo inaonekana kwamba licha ya juhudi hizo za Paris, Watunisia wengi wanaitambua Ufaransa kuwa chanzo cha matatizo mengi yanayoikabili nchi yao hususan kutokana na ukoloni wa Paris wa miaka 75 dhidi ya taifa hilo ambao ulianza mwaka 1881 kwa uvamizi wa kijeshi na kisha kumuunga mkono kikamilifu dikteta Zine El Abidine Ben Ali, rais wa zamani wa nchi hiyo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo kupanuliwa mahusiano ya nchi mbili hizo ukachukuliwa kuwa ni suala gumu katika mazingira ya hivi sasa.