Apr 18, 2017 15:34 UTC
  • Mamia ya mateka wa Boko Haram wakombolewa Nigeria

Jeshi la Nigeria limefanikiwa kukomboa mamia ya mateka waliokuwa wakishikiliwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Nigeria imesema kuwa, mateka 1623 wamekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Boko Haram katika operesheni maalumu iliyofanywa na jeshi katika jimbo la Borno na kwamba magaidi 21 wameangamizwa.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, mateka waliokombolewa wakiwemo watoto, wamehamishiwa katika kambi ya jeshi la Nigeria.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) hivi karibuni ulieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la vitendo vya kundi la Boko Haram vya kutumia watoto wadogo katika mashambulizi yake ya kigaidi. UNICEF imesema kuwa, idadi na watoto wanaofariki dunia katika mashambulizi hayo imeongezeka sana.

Baadhi ya wanawake na watoto waliokombolewa na jeshi al Nigeria

Kundi la Boko Haram lilianza mashambulizi dhidi ya maeneo ya umma na taasisi za serikali huko kaskazkini mwa Nigeria mwaka 2009 na baadaye lilipanua mashambulizi hayo hadi katika nchi za Chad, Cameroon na Niger. Zaidi ya watu elfu 20 wameuwa hadi sasa katika mashambulizi hayo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.   

Tags