Makumi ya Wasudan watangaza himaya yao kwa mateka wa Palestina
Makumi ya wananchi wa Sudan wameandamana na kukusanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa mateka wa Kipalestina.
Waandamanaji hao mbali na kulaani vitendo vya kinyama vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina wanaotaabika katika magereza ya utawala huo ghasibu wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kukomesha vitendo hivyo.
Makumi ya wanachama wa Jumuiya ya Kitaifa ya Vijana, wawakilishi wa vyama vya kisiasa na wafanyakazi wa ubalozi wa Palestina mjini Khartoum wameshiriki katika maandamano na mkusanyiko huo.
Aidha waandamanaji hao wamemkabidhi barua mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan inayotaka ulazima wa uingilijia kati wa haraka wa asasi za kimataifa kwa ajili ya kuwaokoa mateka wa Kipalestina kutoka katika korokoro za utawala dhalimu wa Israel.
Aidha wametaka utawala wa Kizayuni wa Israel ushinikizwe na jamii ya kimataifa ili uheshimu sheria za kimataifa na haki za binadamu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo ukosoaji wa hatua za ukandamizaji za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina zinaendelea kulaaniwa kila kona ulimwenguni huku jamii ya kimataifa ikitakiwa kuchukua hatua za haraka ili kukomesha ukandamizaji huo wa Wazayuni.