Rais Kenyatta aagiza uchunguzi baada ya ajali kuua watu 20 Kenya
(last modified Sat, 13 May 2017 13:53:21 GMT )
May 13, 2017 13:53 UTC
  • Rais Kenyatta aagiza uchunguzi baada ya ajali kuua watu 20 Kenya

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameagiza uchunguzi kufanyika baada ya watu 20 kupoteza maisha Jumamosi asubuhi kufuatia ajali mbaya ya barabarani katika barabara ya Nairobi-Nakuru.

Katika salamu zake za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki kufuatia ajali hiyo ya basi, Rais Kenyatta amebainisha kusikitishwa kwake na watu kupoteza maisha na kuwataka maafisa wa serikali kufanya uchunguzi kubaini chanzo hasa cha ajali hiyo. Katika ujumbe huo aliotuma akiwa safarini nchini China, Rais Kenyatta aidha ametaka hatua zichukuliwe kuhakikisha usalama barabarani unadumishwa.

Katika ajali hiyo, abiria wengine wanaokisiwa kuwa zaidi ya 40 walipata majeraha ya viwango mbalimbali ambapo wamelazwa katika hospitali kadha za Kaunti ya Nakuru.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Nakuru, Hassan Rashid Barua, basi la uchukuzi wa abiria lililokuwa likitoka Nairobi kuelekea Busia lilikuwa likipita trela ambapo lilikumbana na trela nyingine na kugongana ana kwa ana. Alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Soysambu karibu na Mbaruk katika barabara ya Nairobi kuelekea Nakuru.

Ajali za barabarani hutokea nchini Kenya mara kwa mara kutokana na madereva kutozingatia sheria za usalama barabarani.