Wataka mkuu wa jeshi apandishwe kizimbani Libya kwa kushirikiana na Misri
Wanaharakati nchini Libya wametaka mkuu wa jeshi la nchi hiyo apandishwe kizimbani kwa madai ya kula njama na Misri na kutoheshimu haki ya kujitawala Libya.
Siku chache zilizopita, Mkuu wa Jeshi la Misri, Luteni Jenerali Mahmoud Ibrahim Mahmoud Hegazy alisema kuwa, mkuu wa jeshi la Libya, Jenerali Khalifa Haftar ameiruhusu Misri kufanya mashambulizi ya nchi kavu dhidi ya maficho ya magaidi katika mji wa Derna wa mashariki mwa Libya.
Matamshi hayo yameamsha hasira kali kutoka kwa wanaharakati wa masuala ya kijamii na kisiasa wa Libya ambao wametaka Jenerali Khalifa Haftar apandishwe kizimbani kwa madai ya kuisaliti Libya.
Mkuu wa Jeshi la Misri ametoa matamshi hayo sambamba na kuenea habari kwamba jeshi la nchi hiyio linajiandaa kufanya mashambulizi ya nchi kavu kwenye maficho ya makundi ya kigaidi, mashariki mwa Libya.
Mmoja wa wanasiasa wa Libya, Abdul Basit Katit amesema, lengo la Misri ni kuivamia na kuikalia kwa mabavu Libya na si kupambana na magaidi.
Hivi karibuni pia Mkuu wa Jeshi la Misri alionana na mwenzake wa Libya katika mji wa Benghazi. Ijapokuwa lengo la mazungumzo hayo halikutangazwa, lakini duru za Misri zimesisitiza kuwa, ziara hiyo imefanyika katika jitihada za kulisaidia jeshi la Libya kupambana na magenge ya kigaidi.