Kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Chad
Hali ya kibinadamu nchini Chad na hasa magharibi mwa nchi hiyo katika bonde la Ziwa Chad imeripotiwa kuwa mbaya huku hofu ya kuongezeka idadi ya wahajiri na kumiminika wimbi jipya la wakimbizi katika eneo hilo ikitishia kuifanya hali hiyo iwe mbaya zaidi.
Pierre Valiquette, mkuu wa shirika moja lisilio la kiserikali la misaada ya kibinadamu ametahadharisha juu ya kushadidi tatizo la wakimbizi nchini Chad na kutilia mkazo kukidhiwa mahitaji yao akthari ya wakimbizi walioko nchini humo ya kupatiwa misaada ya kibinadamu na hasa bidhaa za chakula.
Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kuwa idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu nchini Chad katika mwaka huu wa 2017 ni milioni nne na elfu 70. Na hii ni katika hali ambayo makadirio yaliyofanywa na umoja huo yanaonyesha kuwa watu milioni 11walioko kwenye eneo la Bonde la Ziwa Chad lililoko magharibi mwa Chad likiunganisha pia nchi nyengine jirani za Cameroon, Niger na Nigeria, wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu.
Kwa miaka kadhaa sasa Chad inakabiliwa na migogoro mbalimbali. Mbali na matatizo ya ndani yakiwemo ya uchumi na kisiasa, masuala mawili ya ugaidi na kukosekana uthabiti wa kisiasa katika nchi za eneo hilo sio tu yameifanya Chad ikabiliwe na tatizo la wakimbizi, lakini kutokana na kuongezeka idadi ya wakimbizi hao na kukosekana suhula, kutokea hali mbaya ya kibinadamu kumekuwa tishio kubwa linaloikabili nchi hiyo na eneo la Bonde la Ziwa Chad kwa ujumla.
Kushamiri harakati za kigaidi hasa za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini Nigeria na kuenea hujuma za kundi hilo katika eneo kumeifanya hali katika nchi nyingi za eneo hilo hasa zile zinazopakana na Bonde la Ziwa Chad iwe ngumu na kuzidisha uwezekano wa kushambuliwa wakaazi wa eneo hilo, kiasi kwamba kuendelea harakati za kigaidi za Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria na maeneo ya karibu yake kumesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa watu waliobaki bila makaazi barani Afrika.
Kutokana na mashambulio na hujuma za kigaidi za Boko Haram, raia wengi wa Nigeria na wa nchi jirani wamelazimika kutafuta hifadhi katika maeneo yenye usalama likiwemo la Bonde za Ziwa Chad. Na hii ni katika hali ambayo, kuongezeka idadi ya wahajiri kwa upande mmoja na uhaba wa bidhaa za chakula na suhula za afya na tiba kwa upande mwengine, kumelifanya eneo la Ziwa Chad likumbwe na hali mbaya ya kibinadamu inayoshtadi zaidi siku hadi siku. Ni kama alivyoeleza Pierre Valiquette, ambaye shirika lake ni miongoni mwa mashirika ya zamani ya misaada ya kibinadamu linaloendesha shughuli zake katika eneo hilo, kwamba umasikini na idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu inazidi kuongezeka nchini Chad.
Kupanuka wigo wa hali mbaya ya kibinadamu katika eneo la Bonde la Ziwa Chad kunashuhudiwa katika hali ambayo ukame umezidisha ukubwa wa maafa katika eneo hilo. Ardhi nyingi za kilimo zimekauka kwa joto la jua na kutonyesha mvua kulikotokana na mabadiliko ya tabianchi na kushindwa kuzalisha mazao yoyote. Licha ya hali kuzidi kuwa mbaya misaada ya kibinadamu inayofikishwa huko pia haitoshi.
Mbali na eneo la Ziwa Chad, kutokuwepo uthabiti wa kisiasa, vita na mapigano ya ndani katika nchi jirani navyo pia vimeifanya Chad yenyewe hasa maeneo yake ya kusini na mashariki yakabiliwe na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na eneo la Darfur la nchini Sudan. Matatizo hayo yakijumuishwa na matatizo ya ndani ya Chad kwenyewe kama kupungua pato la taifa kutokana na kushuka bei ya mafuta, kuongezeka bajeti ya gharama za ulinzi na usalama pamoja na umasikini na ukosefu wa ajira, vimeifanya nchi hiyo ikaribie kukumbwa na hali mbaya ya kibinadamu.
Hali mbaya ya wakimbizi ni mgogoro mkubwa na mpana ambao umezikumba nchi zote za eneo. Inavyoonyesha, mgogoro huo utaweza kutatuka kwa ushirikiano wa nchi zote katika kupambana kwa nguvu zote na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram na vitisho vinavyosababishwa na kundi hilo sambamba na kurejesha amani na uthabiti wa kisiasa katika nchi za Bonde la Ziwa Chad…/