Jun 11, 2017 13:56 UTC
  • Kundi la Boko Haram latangaza kuhusika na shambulio la Maiduguri

Kundi la kigadi la Boko Haram limetangaza kuwa, wanachama wake ndio waliohusika na shambulio la kigaidi la hivi karibuni katika mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Mkanda wa sauti uliotolewa na kundi la Boko Haram unabainisha kwamba, wanachama wa kundi hilo ndio waliohusika na operesheni ya kigaidi ya Jumatatu usiku katika mji wa Maiduguri ulioko katika jimbo la Borno ambapo watu 14 waliuawa.

Mji wa Maiduguri umekuwa kituo cha mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram tangu mwaka 2009.

Hivi sasa kundi hilo la kigaidi limeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya raia na maafisa wa kulinda usalama wa Nigeria.

Rais Muhammadu Buhari ambaye serikali yake imeshindwa kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram

Tangu lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 hadi hivi sasa, genge hilo limeshaua watu wasiopungua 20 elfu na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni mbili na laki sita wengine. Mamia ya maelfu ya watu wamejeruhiwa kwenye mashambulizi ya Boko Haram, kundi ambalo hivi sasa limepanua maeneo ya mashambulizi yake na kuzijumuisha nchi nne jirani za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, ilani kuu ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ilikuwa ni kuliangamiza kundi hilo mara tu baada ya kuingia madarakani.

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari inakosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na kundi la Boko Haram. Hata kikosi cha pamoja cha nchi za eneo kilichoundwa kwa shabaha ya kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram kinaonekana kushindwa kufikia malengo yake. 

Tags