Makumi wauawa katika mapigano ya kikabila katika jimbo la Taraba Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30906-makumi_wauawa_katika_mapigano_ya_kikabila_katika_jimbo_la_taraba_nigeria
Makumi ya watu wanaripotiwa kuuawa katika mapigano ya kikabila yaliyozuka katika jimbo la taraba la mashariki mwa Nigeria huku kikosi maalumu cha askari kikitumwa katika eneo hilo kwa ajili ya kutuliza mambo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2017 09:42 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano ya kikabila katika jimbo la Taraba Nigeria

Makumi ya watu wanaripotiwa kuuawa katika mapigano ya kikabila yaliyozuka katika jimbo la taraba la mashariki mwa Nigeria huku kikosi maalumu cha askari kikitumwa katika eneo hilo kwa ajili ya kutuliza mambo.

Kiongozi mmoja wa jumuiya ya wafugaji nchini Nigeria amesema kuwa, mapigano hayo yaliyodumu kwa siku tano sasa katika jimbo la Taraba lililoko katika mpaka wa nchi hiyo na Cameroon yamepelekea wafugaji 105 ambao ni Waislamu wa kabila la Fulani kuuawa.

Mapigano hayo ambayo inaelezwa kuwa chanzo chake ni mizozo ya malisho ya mifugo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu na kuzua wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia wa maeneo hayo.

Zaidi ya nyumba 100 zimechomwa moto katika vurugu na ghasia hizo za kikabila ambapo maelfu ya mifugo wameibiwa na wengine wakiuawa. Ripoti zaidi zinasema kuwa, kufuatia kutanda hali ya wasiwasi, juzi serikali ya Nigeria ilituma kikosi maalumu cha askari katika jimbo hilo ili kwenda kutuliza mambo.

Ramani ya Nigeria ikionyesha makabila ya nchi hiyo sehemu yalipo

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Kaimu Rais wa Nigeria, Profesa Yemi Osinbajo hivi karibuni alikutana na viongozi wa maeneo kadhaa kujaribu kuzima malumbano ya kikabila yanayotokota katika nchi hiyo.

Aidha siku za hivi karibuni zimeshuhudia kuongezeka machafuko baina ya wakazi wa kaskazini mwa Nigeria wa kabila la Hausa na wale wa kusini mashariki wa kabila la Igbo. Makabila ya Kaskazini mwa Nigeria yanayowajumuisha Wafulani, Wahausa na Waberom yanataka Waigbo watimuliwe kaskazini mwa nchi hiyo kwa sababu ya harakati zao za uasi wa kutaka kujitenga na kuunda taifa lao la Biafra kusini mashariki mwa nchi.