Jul 04, 2017 03:45 UTC
  • Boko Haram wafanya shambulizi jingine kusini mashariki mwa Niger

Watu 9 wameuawa katika shambulio jipya lililofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram, kusini mashariki mwa Niger.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu mmoja wa mameya wa miji ya Niger anayejulikana kwa jina la Abagana Isa akisema jana kuwa, wanamgambo wa Boko Haram usiku wa kuamkia Jumatatu walikivamia kijiji cha Ngalewa katika eneo la Diffa la kusini mashariki mwa Niger na mbali na kuua raia tisa, wamewateka nyara karibu wanawake na watoto wadogo wapatao 40.

Kwa upande mmoja Niger inakabiliwa na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram na upande mwingine inakabiliwa na mashambulizi ya watu wenye misimamo mikali katika mpaka wa mashariki mwa nchi hiyo yaani katika mpaka wake na Mali.

Operesheni ya kupambana na magaidi wa Boko Haram nchini Niger

 

Genge la Boko Haram lilianzisha mashambulizi kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu za Magharibi, lakini mwaka 2015 lilipanua wigo mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Ni hivi karibuni tu ambapo kundi la kigadi la Boko Haram lilitangaza kuwa, wanachama wake ndio waliohusika na shambulio la kigaidi lililotokea katika mji wa Maiduguri wa kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Mkanda wa sauti uliotolewa na kundi la Boko Haram ulisema kuwa, wanamgambo wa genge hilo la kitakfiri ndio waliohusika na shambulio la kigaidi la mwanzoni mwa mwezi Juni katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, shambulizi ambalo liliua watu 14.

Tags