Kukombolewa Benghazi, Khalifa Haftar azidi kujiimarisha
Kukombolewa Benghazi, mji wa pili kwa ukubwa wa Libya ambao umekuwa ukikaliwa na makundi ya kigaidi kwa kipindi cha miaka mitatu kumetajwa kuwa huenda kukaimarisha zaidi nafasi na Jenerali Khalifa Haftar na kumkurubisha zaidi kwenye udhibiti na madaraka ya Libya.
Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya, Jenerali Haftar alitangaza Julai 5 kwamba vikosi vya jeshi hilo vimefanikiwa kudhibiti kikamilifu mji wa Benghazi baada ya vita na mapigano ya miaka 3 dhidi makundi ya kigaidi. Khalifa Haftar ameyataja mafanikio hayo kuwa ni ushindi mkubwa dhidi ya ugaidi na kusisitiza kuwa, Benghazi imekombolewa kikamilifu kutoka kwenye makucha ya magaidi.
Umuhimu na nafasi ya mji wa Benghazi imelifanya tukio la kukombolewa kwake kuwa hatua kubwa ya kurejeshwa amani na usalama nchini Libya. Kihistoria mji wa Benghazi ndio uliokuwa mji mkuu wa Libya kabla ya Tripoli na ndio mji wa pili kwa ukubwa nchini humo. Mji huo pia unapewa umuhimu mkubwa kwa kuzingatia kwamba, ndio uliokuwa kituo kikuu cha mapinduzi ya wananchi mwaka 2011 yaliyoiondoa madarakani serikali ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Katika upande wa kiuchumi pia mji wa Benghazi una umuhimu mkubwa kutokana na kuwa na bandari kubwa ambayo kazi zake zilismamishwa mwaka 2014 baada ya kudhibitiwa na makundi ya kigaidi.
Mji huo muhimu sasa umekombolewa kutoka kwenye makucha ya kundi linalojiita Baraza la Mapinduzi lenye mfungamano mkubwa na kundi la kigaidi la Daesh baada ya vita na mapigano ya miaka mitatu. Kukombolewa mji huo kuna maana kwamba, magaidi wa Libya pia wameanza kusambaratika na kudhoofika. Hata hivyo jambo la kutiliwa maanani zaidi ni kuwa, Benghazi imekombolewa na Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na si vikosi vya jeshi la al Fayez Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa. Awali Jeshi la Khalifa Haftar pia lilikuwa limefanikiwa kukomboa kikamilifu mji wa Sirte na kusambaratisha kundi ya kigaidi linalojiita Ansaru Shari'a lenye uhusiano mkubwa na Daesh. Kwa msingi huo mafanikio ya Jenerali Khalifa Haftar katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Libya yanaimarisha zaidi nafasi yake nchini humo. Suala hili kwa upande mwingine linatoa changamoto kubwa kwa mchakato wa kurejesha amani na kuundwa serikali moja nchini humo.
Libya ina serikali mbili na mabunge mawili yanayokinzana na juhudi zilizofanywa na jamii ya kimataifa kwa ajili ya upatanishi na kuundwa serikali moja yenye nguvu hazijazaa matunda ya kuridhisha.
Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, japokuwa kushindwa kwa makundi ya kigaidi na kukombolewa mji wa Benghazi huko Libya ni tukio zuri na muhimu, lakini ushindi huo uliopatikana kwa uongozi wa Khalifa Haftar utadhoofisha serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyotokana na makubaliano ya Disemba 2015 ya Skhirat mkabala wa serikali na Bunge la Tripoli.