Shambulio la kigaidi nchini Burkina Faso
Serikali ya Burkina Fasso imetangaza kuwa, zaidi ya watu 18 wameuawa na wengine 8 kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotokea katika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.
Taarifa ya vyombo vya usalama inasema kuwa, genge la watu wenye silaha limeua raia wasiopungua 18 na kujeruhi wengine 8 baada ya kuvamia na kushambulia hoteli moja ya kigeni ya Kituruki katika mji mkuu huo. Shambulio hilo linashabihiana na lile lililofanyika Januari mwaka jana dhidi ya Hoteli za Splendid na Cappuccino mjini Ouagadougou ambapo watu wapatao 30 waliuawa.
Licha ya kuwa, kwa muda sasa Burkina Faso ilikuwa ikihesabiwa kuwa moja ya nchi zenye amani na usalama katika ukanda wa magharibi mwa Afrika, lakini katika miaka ya hivi karibuni, nchi hiyo nayo imekumbwa na harakati za makundi ya kigaidi. Kuwa na mpaka mpana na nchi za Niger na Mali na kushiriki kikosi cha Burkina Faso katika vita dhidi ya ugaidi, ni miongoni mwa sababu zilizopelekea nchi hiyo nayo izingatiwe na makundi ya kigaidi.
Harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram katika eneo la magharibi mwa Afrika hususan nchini Nigeria, kwa miaka mingi sasa zimevuruga amani na uthabiti wa eneo hilo. Licha ya kuweko juhudi zote za kupambana na kundi hilo la kigaidi, lakini hadi sasa juhudi hizo hazijafuadafu na badala yake kundi hilo limepanua zaidi wigo wa mashambulio yake hadi katika nchi jirani kama Niger na Cameroon.
Katika upande mwingine tatizo la ukosefu wa usalama nchini Mali nalo limeandaa anga ya kuibuka makundi mapya ya kigaidi na hivyo kupelekea kupanuka harakati za makundi ya kigaidi katika eneo hilo. Kiasi kwamba, kuendelea hali hii kumezidisha tishio la kupanuka harakati za kigaidi katika nchi nyingine ambazo kwa namna fulani zina amani na usalama kwa kiwango fulani.
Kuhusiana na jambo hilo, hivi karibuni Mohamed Ibn Chambas, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika eneo la magharibi mwa Afrika alitahadharisha kwamba: Kuendelea mashambulio ya mauaji katika maeneo ya mpakani ya Mali kumezidisha hatari ya mapigano hayo kuvuka mipaka na kuingia katika nchi za Burkina Faso na Niger.
Hii ni katika hali ambayo, ni kwa muda sasa ambapo nchi za eneo hilo zimekuwa zikitekeleza mipango mbalimbali yenye lengo la kukabiliana na harakati za makundi ya kigaidi katika eneo hilo, ambapo ushirikiano wa kulinda mipakani na wa kieneo ni miongoni mwa mipango hiyo. Aidha katika uwanja huo, hivi karibuni kulichukuliwa uamuzi wa kuanzishwa kikosi cha kundi la nchi tano za eneo la Sahel Afrika kwa shabaha ya kupambana na ugaidi. Kikosi hicho kinaundwa na nchi za Mauritania, Mali, Burkina Faso, Chad na Niger na jukumu lake kuu ni kupambana na makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati katika maeneo hayo.
Amadou Alpha ly, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kijamii barani Afrika anasema kuwa: Kikosi cha pamoja cha kundi la nchi tano za eneo la Sahel Afrika kitapunguza harakati za makundi ya kigaidi katika eneo hilo na kuwa na nafasi muhimu katika vita dhidi ya ugaidi katika eneo hilo la Afrika.
Kwa hakika ushirikiano wa nchi za eneo hilo kwa ajili ya kupambana na ugaidi, kuwafuatilia na kuwasaka wanachama wa makundi ya kigaidi, umepelekea akthari ya makundi ya kigaidi kukabiliwa na vizingiti katika harakati zao. Makundi hayo nayo yakiwa na lengo la kutoa jibu kwa vizuizi hivyo, yamepanua harakati zao katika nchi mbalimbali za Afrika Magharibi.
Shambulio la kigaidi la Burkina Faso nalo linaweza kutambuliwa kama pigo kwa viongozi wa nchi hiyo ambao nchi yao inashiriki katika vita dhidi ya ugaidi. Lengo jingine la shambulio hilo ni kuzusha hofu na wahaka miongoni mwa nchi za eneo hilo.
Pamoja na hayo, filihali nchi za magharibi mwa Afrika zina matumaini ya kupata ushindi katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi katika eneo hilo kuliko wakati mwingine wowote ule.