Mashauriano ya wawakilishi wa Afrika na Ufaransa katika "Kikao cha Afrika 2017"
Kikao cha siku mbili chini ya anuani "Afrika 2017" kimefanyika kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili za Afrika na Ufaransa.
Wawakilishi wa kisiasa na kisheria kutoka nchi za Afrika zaidi ya 30 pamoja na viongozi wa ngazi ya juu wa Ufaransa wamezungumzia masuala na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika katika kikao hicho cha siku mbili kilichofanyika katika ngazi ya kimataifa kwenye miji mikuu mitatu ya Ivory Coast, Kenya na Tunisia yaani huko Abdijan, Nairobi na Tunis.
Kikao hicho kimefanyika huku nchi mbalimbali za bara la Afrika zikikabiliwa na changamoto kubwa nyingi. Hatua ya baadhi ya viongozi wa nchi za bara hilo ya kushindwa kuheshimu demokrasia katika nchi zao kufikia hadi ya kufanyiwa marekebisho katiba za nchi hizo ili waendelee kutawala; ni mambo ambayo yamekumbwa na upinzani na ukosoaji mkubwa wa vyama vya siasa. Hatua hiyo ya kubadilisha katiba pia imekuwa ikichochea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi mbalimbali za bara la Afrika. Kwa mfano wakati kikao hiki kilipokuwa kinafanyika huko Nairobi, mji huo ulikumbwa na maandamano ya wapinzani wa serikali wanaoshinikiza kufanyiwa marekebisho Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC). Matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika Agosti Nane mwaka huu yalibatilishwa kufautia malalamiko yaliyowasilishwa na upande wa upinzani na uchaguzi wa marudio umepangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, hata hivyo wapinzani wanalalamika namna uchaguzi huo utakavyoendeshwa.
Kuongezeka makundi ya wanamgambo na ya kigaidi sambamba na kuenea ukosefu wa amani na machafuko ni masuala mengine yanayovuruga utulivu katika nchi nyingi za bara la Afrika. Suala la vita dhidi ya makundi ya kigaidi barani Afrika linatumiwa kama wenzo wa kujiimarisha kijeshi barani humo baadhi ya nchi ikiwemo Ufaransa. Wanajeshi wa Ufaransa wapo katika nchi nyingi za bara hilo zikiwemo Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ukame na hali mbaya ya kiuchumi inavyosababisha ukosefu wa ajira na umaskini ni matatizo mengine yanazozitesa nchi za bara hilo.
Historia inaonyesha kuwa nchi za bara la Afrika zimekoloniwa na Ufaransa na Wafaransa wamekuwa wakihusika na masuala mbalimbali ya nchi hizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Katika zama hizi mpya na licha ya nchi za Afrika kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Magharibi ikiwemo Ufaransa, lakini utajiri mkubwa wa maliasili za nchi hizo kama vile madini, nguvu kazi kubwa na ya gharama nafuu, nafasi nzuri ya kisiasa-kijiografia ya nchi za Afrika yote hayo yamezifanya nchi mbalimbali za bara hilo ziendelee kuwa mahali pa ushindani wa madola makubwa ya Magharibi yanayomenyana vikali kwa ajili ya kuendelea kuwa na ushawishi barani humo.
Ibrahim Hamidu Mwandishi habari wa Ngeria anasisitiza namna Ufaransa inavyopigania kulinda uhusiano wa kiutamaduni na kiuchumi uliobakizwa wakati wa ukoloni barani humo na kueleza kuwa hakuna mtawala yoyote wa Ufaransa ambaye hadi sasa ameonekana kupinga kukoloniwa Afrika.
Rekodi ya nafasi ya Ufaransa barani Afrika inaashiria kuwa, kuwepo nchi hiyo barani humo hakujasadia kuleta maendeleo, wala utulivu na usalama katika nchi za bara hilo, bali mara zote imekuwa inahalalisha kujipenyeza na kujizatiti barani humo kwa maslahi yake binafsi.
Hivi sasa pia hata kama lengo la kufanyika kikao hicho limetajwa kuwa ni kuzidisha ushirikiano wa kibishara na kiuchumi kati ya Afrika na Ufaransa, lakini rekodi ya mkoloni mkongwe Ufaransa barani Afrika inaonyesha kuwa kuwepo nchi hiyo ya Ulaya barani humo ni kwa ajili tu yakujiimarisha zaidi nchi hiyo katika zama hizi mpya.