16 wauawa katika mapigano na polisi nchini Msumbiji
Watu 16 wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia vituo vya polisi katika mji mmoja mdogo wa kaskazini mwa Msumbiji. Polisi wawili na watu 14 wenye silaha wameuawa katika mlolongo wa mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi katika mji mdogo wa Mocimboa de Praia, kaskazini mwa Msumbiji.
Mashambulizi hayo yalianza siku ya Alkhamisi, hata hivyo habari zinasema kuwa, maafisa wa Msumbiji wanacherewa sana kutoa taarifa kuhusu mapigano yaliyosababishwa na uvamizi huo wa vituo vya polisi.
Kwa mujibu wa habari ya jana Jumamosi ya maafisa hao, watu 14 wenye silaha wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na kwamba mashambulizi dhidi ya vituo hivyo vya polisi yalikuwa yamepangwa vyema tangu zamani.
Vyombo vya habari vya Msumbiji vimetangaza kuwa, vituo vitatu vya polisi vya mji huo wenye utajiri wa gesi asilia vimeshambuliwa na watu wenye silaha.
Hadi hivi sasa polisi wa Msumbiji wameshawatia mbaroni watu 10 na kukamata silaha nne na risasi 100.
Waandishi wa habari wa ndani ya Msumbiji wamesema kuwa washambuliaji hao ni kutoka kundi lisilojulikana. Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, mapigano hayo yamedumu kwa muda wa siku mbili kiasi kwamba serikali ya Msumbiji imelazimika kutuma askari maalumu kutoka mjini Pemba, umbali wa kilomita 500 kutoka eneo la tukio, kwenda kuwasaidia askari wa mji huo.
Katika miaka ya hivi karibuni kumezuka mapigano mengi baina ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo watiifu kwa chama cha upinzani cha waasi wa zamani wa Renamo huko Msumbiji.